Customer Feedback Centre

Ministry of Health

WARATIBU WA MAABARA WATAKIWA KUVISAIDIA VITUO KUTOA HUDUMA BORA

Posted on: June 27th, 2023

Na WAF Dodoma

Mwenyekiti wa bodi ya Maabara binafsi za Afya na Mkurugenzi wa huduma za Tiba Wizara ya Afya, Prof. Pascal Ruggajo amewataka waratibu wa mikoa wa maabara kuwasaidia wamiliki wa maabara kutoa huduma bora ili kuleta katika kuwahudumia wananchi.

Prof. Pascal ametoa agizo hilo leo wakati akifungua mkutano wa mwaka wa waratibu huduma za maabara ngazi ya Mkoa unaofanyika kwa siku Mbili Mkoani Dodoma wenye lengo la kupokea taarifa za utekelezaji wa usimamizi wa huduma za maabara kwenye mikoa

Amesisitiza waratibu hao kutokuwa wakamataji na wafungiaji ila wahakikishe wanafanya vikoa vya mara kwa mara ambavyo vitakuwa na chachu ya kuboresha, kuwajengea uwezo na kuwahamasisha kutoa huduma bora kwa jamii.

Prof. Ruggajo amesema, wanahitaji maabara bora nchini zitakazo toa vipimo bora kwahiyo ukosefu wa kufanya vikao na wamiliki ndio mwanzo wa wao kujiona kama watuhumiwa na kuiona serikali kama polisi na hilo linapoteza lengo la msingi la kufikisha huduma bora kwa watanzania .

"Wapo ambao pengine wana mapungufu kidogo ambayo yakirekebishwa yanaleta matokeo chanya ya kutoa huduma za uchunguzi ukimuacha bila msaada muda mwingine ukirudi utakuta hajatimiza vigezo na unamfungia ambapo wananchi wa eneo hilo itabidi watembee umbali mrefu kufuata huduma" Ameeleza Prof. Ruggajo

Aidha, Prof. Ruggajo amewataka Waratibu hao kuweka mipango ya ufuatiliaji wa huduma za maabara ili kuimarisha ubora wa huduma za maabara ikiwemo kuhakikisha maabara zote zinaajiri wataalamu walio na sifa, kuhakikisha maabara zinafanya sampuli za uhakiki ubora (IQC) ii kuhakiki ubora wa majibu kwa wagonjwa pamoja na kudhibiti maabara zinazoendeshwa kiholela bila usajili.

Pia, Prof. Ruggajo amesema kuwa kwa kipindi cha mwezi Julai 2022 hadi Juni 2023 jumla ya maabara binafsi mpya 303 zilisajiliwa katika maenco mbalimbali nchini, hivyo kufanya jumla ya maabara zipatazo 3,212 kati ya hizo 1,619 zimejishikiza Katika vituo vya kutolea huduma za afya na 1,593 zinajitegemea.