Customer Feedback Centre

Ministry of Health

Wamachinga,Mama Lishe jijini Mwanza wajengewa uelewa kuhusu Bima ya Afya kwa Wote

Posted on: January 4th, 2023

Na. WAF - Mwanza


Serikali kupitia Wizara ya Afya imewajengea uelewa kuhusu Bima ya Afya kwa wote viongozi wa  makundi ya Wamachinga, Wakulima, Wavuvi, Wachimba Madini, Bodaboda, Mama Lishe na Kamati ya Amani ya Mkoa wa Mwanza ili wakawe Mabalozi wa kutoa elimu ya Bima ya Afya kwa Wote katika jamii.


Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya wakati akifungua kikao kazi cha kutoa Elimu ya Bima ya Afya kwa Wote kwa makundi mbalimbali jijiji Mwanza


"Sasa tunakuja na maboresho ya Bima ya Afya ambayo itakua ni Bima ya Afya kwa Wote, kila mtu kwa hali yake ya kiuchumi aingie kwenye mfumo wa Bima ya Afya hii". Amesema Prof. Makubi.


Ameeleza kuwa Muswada wa Bima ya Afya kwa Wote ukipitishwa utaongeza wigo wa wananchi wengi kujiunga katika mfumo wa Bima ya Afya  kutoka asilimia 15 ya sasa mpaka asilimia 70 na kuendelea ya Watanzania.“Serikali  makini haiwezi kuacha makundi yote haya muhimu wabaki bila kuwa na uhakika wa matibabu ya afya zao.Hivyo lazima kuweka mpango wa Bima ya Afya kwa wote ambapo mtu akiugua kwa hali yoyote ya kifedha aliyonayo aweze kutibiwa kwa haraka na wakati ili aendelee na shughuli zake za utafutaji"Aliongeza Prof. Makubi