Customer Feedback Centre

Ministry of Health

WAGONJWA WA MOYO ZAIDI YA 800 WAFANYIWA UPASUAJI MKUBWA

Posted on: February 9th, 2024


Na, WAF - Zanzibar


Wagonjwa wa moyo zaidi ya 800 wamefanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo huku wengine zaidi ya 2,000 kufanyiwa upasuaji wa tundu dogo kwa kutumia mtambo wa ‘cathlab’ kwa kipindi cha miaka Miwili katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).


Hayo yamesemwa leo Februari 9, 2024 na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango wakati akifungua mkutano wa Kimataifa wa magonjwa ya moyo mjini Zanzibar.


“Lakini pia, wagonjwa wa moyo zaidi ya laki mbili wamepatiwa matibabu katika Taasisi hiyo kwa kipindi cha miaka miwili ambapo kati yao wagonjwa 2,400 walitoka nchi za jirani za Comoro, Congo DRC, Kenya, Malawi, Mozambique, Rwanda, Uganda pamoja na Zambia.” Amesema Dkt. Mpango 


Amesema, kutokana na huduma zinazotolewa na Taasisi hiyo zimeweza kuifanya JKCI kuwa Taasisi ya umma inayoongoza katika kutoa huduma za matibabu ya moyo Afrika Mashariki na kati hivyo kuwavutia wanataaluma kutoka nchi za jirani zikiwemo nchi za Malawi, Zambia na Rwanda kujenga mashirikiano.


Aidha, Mheshikiwa Makamu wa Rais Dkt. Mpango amesema kupitia Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Serikali imeweza kuokoa Tsh: Bilioni 63 fedha za Kitanzania zilizokuwa zinatumika kwa ajili ya matibabu ya moyo nje ya nchi.


“Kati ya mafanikio yaliyofanywa na Taasisi hiyo ni pamoja na uanzishwaji wa kambi maalumu ya matibabu ya moyo ijulikanayo kwa jina la Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan services ambayo imekuwa ikitoa huduma ya kuwajengea uwezo wataalamu wa Afya waliopo katika hospitali za mikoa na kuwafikishia karibu huduma za matibabu ya moyo wananchi wanaohitaji matibabu hayo.” Amesema Dkt. Mpango 


Pia amesema, Serikali itaendelea kuwekeza kakika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kwa kupanua huduma za matibabu na kumtaka Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu kufuatilia gharama za ujenzi utakaofanyika JKCI Dar Group na kuziwasilisha Serikalini mapema ili serikali iweze kuwekeza katika ujenzi huo.


Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge amesema JKCI imeanzisha mkutano huo wa kisayansi kwa wataalamu wa Afya nchini ukiwa na lengo la kuwapa ujuzi wataalamu wa afya nchini kuhusu magonjwa ya moyo.


“Mkutano wetu unahusisha huduma za awali kabisa ambazo mgonjwa wa moyo anatakiwa kupata lengo likiwa kuokoa maisha ya wagonjwa wa moyo kwani wengi wao hufika JKCI kwa kuchelewa.” Amesema Dkt. Kisenge