Customer Feedback Centre

Ministry of Health

WAGANGA WA KIENYEJI SIO SULUHU YA MATIBABU YA KIFUA KIKUU

Posted on: November 3rd, 2023


Kukosekana kwa elimu ya Wataalam wa afya waliobobea katika kuwahudumia wagonjwa kila siku, imewafanya baadhi ya Wananchi kwenda kwa waganga wa kienyeji kupata tiba za ugonjwa wa Kifua Kikuu wakidhani kuwa wamerogwa.


Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Hospitali Maalumu ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi Kibong’oto Dkt. Leonard Subi wakati akizungumza kwenye ufunguzi wa zoezi la upimaji wa ugonjwa wa Kifua Kikuu, Virusi vya Ukimwi, shinikizo la damu, zoezi lililofanyika katika kitongoji cha Orengetwa Kata ya Sanya Juu Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro.


Dkt. Subi amesema kukosekana kwa elimu hiyo, imesababisha baadhi ya Wananchi kukimbilia kwa waganga wa kienyeji wakidhani wamerogwa kabla hawajagundua kama wanaumwa Kifua Kikuu.


"Licha ya serikali kuendelea kutoa elimu kwa Wananchi kwenda kwenye vituo vya afya kupima afya zao, pindi wanapoona dalili za Kifua Kikuu wako baadhi ya Wananchi huenda kwa waganga wa kienyeji kupata tiba hiyo, jambo ambalo limetusukuma sisi kutoka katika kituo chetu cha kazi, kwenda vijijini kwa ajili ya kutoa elimu hii". Amesema Dkt. Subi.


Dkt. Subi amesema takwimu zinaonyesha kuwa watu zaidi ya milioni 10.4 wanaugua Kifua Kikuu kila mwaka na kati yao watu milioni 1.6 wanafariki dunia kutokana na ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB) na nchi ya Tanzania inatajwa kuwa ni miongoni mwa nchi duniani yenye maambukizi ya Kifua Kikuu ambayo yako juu.


"Pamoja na jitihada za ugonjwa wa Kifua Kikuu kupungua , bado kuna wagonjwa wa Kifua Kikuu ambao wako kwenye jamii na wale wanaowagundua ni asilimia 65 tu, huku asilimia 35 wako kwenye jamii na hao ndiyo tunawatafuta ili waweze kupatikana kwa lengo la kuwaweka kwenye matibabu". Amesema.


Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Siha Dkt. Paschal Mbota amesema Wilaya ya Siha ina vituo vya kutolea huduma za afya 27 na kati ya hivyo vituo 12 vinauwezo wa kupima ugonjwa wa Kifua Kikuu


Aidha, Dkt. Mbota amesema kadri ambavyo wamekuwa wakifanya zoezi la upimaji wa ugonjwa wa Kifua Kikuu wamekuwa wakiwaibua wagonjwa wengi wa Kifua Kikuu na kuwapatia matibabu jambo ambalo limesaidia kupunguza kasi ya kuenea kwa ugonjwa huo.