VITUO VYOTE VYA AFYA VIWE NA MKATABA WA HUDUMA BORA KWA MTEJA
Posted on: June 25th, 2025
Na WAF - Dodoma
Vituo vyote vinavyotoa huduma za afya nchini vimetakiwa kuwa na mkataba wa huduma bora kwa mteja ili wananchi na watoa huduma wajue haki na wajibu wao wa kutoa na kupokea huduma kwa uwazi ikiwa ni pamoja na gharama ili kutoa huduma zenye viwango bora vinavyotakiwa.
Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema hayo leo Juni 25, 2025 wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa Mkataba wa Huduma Bora kwa Mteja ambao umefanyika katika ofisi za Wizara ya Afya Jijini Dodoma na kuhudhuriwa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalaghe pamoja na wakurugenzi wa wizara.
"Ndani ya muda mfupi sana, nataka kuona vituo vyote nchini vinavyotoa huduma za afya iwe ni zahanati, kituo cha Afya, hospitali ya wilaya, hospitali zote za rufaa za mikoa, kanda, taasisi zote ndani ya muda mfupi kuhakikisha zinakamilisha mkataba wake wa huduma bora kwa mteja," amesema Waziri Mhagma.
"Ni matarajio yangu, kila mmoja akitimiza wajibu wake kupitia mkataba huu, tutapunguza malalamiko ambayo hayana msingi na tutafika kwenye eneo ambalo Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan anataka kuifikisha Sekta ya Afya," amesema Waziri Mhagama.
Amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amewekeza katika kusomesha watumishi wa sekta ya afya kwenye eneo la ubingwa na ubingwa bobezi pamoja na kuongeza vifaa tiba ikiwemo MRI, PET- Scan, X-Ray mashine ambapo nchi nyingine hawana vifaa hivyo.
Aidha, Waziri Mhagama amesema kupitia mkataba huo utasaidia kutekeleza dira ya Wizara ya Afya ya kuwa na jamii bora yenye ustawi ambayo itachangia kikamilifu katika maendeleo binafsi ya nchi pamoja na dhima ya kutoa huduma bora za afya unaokubalika na zenye uwiano sawa.
"Kazi kubwa tuliyobakiwa nayo sasa ni kuhakikisha mwananchi anapata huduma bora bila kikwazo cha fedha na sasa tumeanzisha Bima ya Afya kwa Wote pamoja na upatikanaji wa fedha ili tuendelee na uwekezaji katika sekta ya afya," amesema Waziri Mhagama.
Pia, Waziri ameelezea miongoni mwa huduma zilizotajwa katika mkataba huo ni pamoja na ushauri wa kitaalam kuhusu uendeshaji wa shughuli za kiafya, masuala ya chanjo, vyeti vya usajili wa kitaaluma, leseni, vibali pamoja na taarifa za sekta ya afya.
"Kupitia mkataba huu wa huduma bora kwa mjeta, niwathibitishie Wizara ya Afya tumejipanga vizuri katika kuyatekeleza hayo kwa ubora unaotakiwa ili mwananchi anapoenda kupata huduma apate huduma iliyo bora na kwa wakati unaotakiwa," amesema Waziri Mhagama.