VITUO VYA DHARURA 39 NDANI YA MIEZI 24 VYAJENGWA
Posted on: August 26th, 2024
Na WAF - MWANZA
Kwa kipindi cha Miaka miwili pekee Serikali imejenga Vituo vipya 39 vya kutolea huduma za dharura za upasuaji hususani kwa wamama wajawazito na kuviekea vifaa tiba katika Mikoa ya kanda ya Ziwa ili kuendeleza adhma yake kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na Watoto wachanga Nchini.
Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa huduma za Afya ya uzazi na mtoto kanda ya Ziwa, Dkt. Fabian Massaga Agosti 26, 2024 Mkoani Mwanza wakati wa mkutano wa Kanda kujadili mikakati ya kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na Watoto wachanga, Mkutano ambao umekutanisha wawakilishi mbalimbali toka Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Hospitali ya Taifa, Hospitali maalumu, Hospitali za Kanda, Mikoa na Halmashauri.
“Huduma za dharura za upasuaji kwa kipindi cha mwaka 2020 hadi 2022 zimeimarika kufuatia ongezeko la vituo ambavyo vimeongezeka kutoka 115 hadi kufikia 149 Katika Mikoa ya kanda ya ziwa Aidha, Serikali imepeleka vifaa tiba katika vituo hivyo na inaendelea kuajiri watumishi wa kada mbalimbali wakiwemo madaktari, wauguzi na tiba saidizi ili kuendana na mahitaji katika vituo vya kutolea huduma za afya” amesema Dkt. Massaga
Ameongeza kuwa Vipo viashiria mbalimbali vinavyoonyesha kuimarika kwa hali ya ubora wa huduma kwa kila mkoa wa kanda ya Ziwa ambapo kwa sasa huduma za wajawazito kuwahi kliniki kabla ya mimba kufikia wiki 12 zimeimarika na kuongeza idadi ya wanaojifungulia katika vituo vya kutolea huduma, na kuongeza idadi za
vituo vyenye uwezo wa kufanya upasuaji na kuimarisha huduma za mama baada ya kujifungua,
Pia amelezea manufaa ya kuimarik kwa huduma hizo kwa mikoa ya kanda ya ziwa ni pamoja na kufanikiwa kwa kiasi kikubwa kupunguza vifo vya wajawazito vitokanavyo na uzazi.
“Katika Kanda yetu ya ziwa kwa miaka minne mfululizo imeweza kupunguza vifo vya wazazi kutoka vifo 420 kwa mwaka 2020 hadi vifo 386 kwa mwaka 2023, Aidha idadi ya kinamama wanaojifungua katika vituo vya kutolea huduma imeongezeka kutoka 572,802 kwa mwaka 2020, hadi 692,037 kwa mwaka 2023, hii ni kutokana na kazi nzuri zinazofanywa na serikali chini ya wizara zetu mbili wizara ya Afya na Tamisemi kwa kushirikiana na viongozi na watendaji wakuu vituoni” amesema Dkt. Massaga
Kwa upande wake Muwakilishi kutoka Wizara ya Afya Dkt. Macdonald Ulimbakisye kutoka idara ya Mama na mtoto ametumia kikao hiko kuwaasa watoa huduma na wataalamu wa Sekta ya Afya nchini kuzingatia uadilifu na uwajibikaji hasa kwa kuzingatia lugha za staha kwa wagonjwa na wateja ili Kuboresha zaidi hali ya utoaji wa huduma na hatimaye kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi vinavyoepukika.