Customer Feedback Centre

Ministry of Health

UTARATIBU WA BIMA YA AFYA NI KUCHANGIANA SIO LAZIMA MPAKA UUGUE” – DKT. MOLLEL

Posted on: September 25th, 2023

Na. WAF – Dar es Salaam


Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amesema lengo la kuwepo na Mifuko ya Bima ya Afya ni wananchi kuchangiana gharama za matibabu kabla ya kuugua ili kuepusha familia hasa za masikini kwa kutumia fedha nyingi kugharamia matibabu.


Dkt. Mollel amesema hayo leo Septemba 25, 2023 jijini Dare Es Salaam wakati akiongea na Vyombo vya Habari ili kuelezea mafaniko ya Sekta ya Afya katika kipindi cha miaka miwili ya Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.


"Katika kipindi cha awamu zote sita, Serikali imefanikiwa kuboresha Sekta ya Afya kwa ujumla, changamoto kubwa iliyobaki na inawayolikabili kundi kubwa la wananchi ni namna ya kuwawezesha kugharamia huduma za afya. Kwahiyo, ili kufikia dhamira ya Serikali ya Afya Bora kwa Wote ni lazima kama nchi kuwa na mfumo endelevu na imara wa uchangiaji wa gharama za matibabu kabla ya kuugua (Bima ya Afya)". Amesema Dkt. Mollel.


Aidha, Dkt. Mollel amesema Mwaka 2016 Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ulianzisha mpango wa bima ya afya kwa watoto walio chini ya miaka 18 (Toto Afya Kadi) kwa lengo la kuwezesha kundi la watoto kwa ujumla wao kujiunga kupitia shule za awali, msingi na sekondari ili kunufaika na mpango huo.


“Hata hivyo, pamoja na uhamasishaji uliofanyika kwa kupindi cha takriban miaka saba (7) bado mwitikio haukuwa wa kuridhisha kwani idadi ya watoto waliojiandikisha ilikuwa ni 210,000 kati ya lengo la watoto milioni 25 kwa kipindi hicho”. Amesema Dkt. Mollel


Dkt. Mollel ameongeza kuwa, kupitia uandikishaji wa kundi hilo, asilimia 99 ya watoto walioandikishwa walikuwa tayari na matatizo ya kiafya ambapo kati ya takriban shilingi bilioni 5 zilizokusanywa kama michango yao, shilingi bilioni 40 zilitumika kugharamia matibabu hali iliyoenda kinyume na dhana na misingi ya uendeshaji wa mfumo wa bima ya afya.


Mwisho, ametoa rai kwa wananchi wote ambao bado hawajajiunga na utaratibu wa bima, wajiunge sasa na pia pindi maamuzi yatakapofanyika ya kupitishwa kwa Bima ya Afya kwa wote wajitokeze kwa wingi kujiunga na Mfumo huu.