Ministry of Health

USHIRIKISHWAJI WA JAMII, KUIMARISHA MIFUMO YA UFUATILIAJI YAFANIKISHA UDHIBITI WA MARBURG

Posted on: March 13th, 2026

Na WAF - Kagera


Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefanikiwa kudhibiti Marburg kwa kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji wa magonjwa, kufanya utambuzi wa haraka wa wagonjwa na kufuatilia watu wote waliokutana na wagonjwa kwa kuwashirikisha wananchi. 


Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Dharura na Maafa kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Erasto Sylvanus, kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Serikali amesema hayo Machi 10, 2026 wakati wa ziara ya Naibu Balozi wa Serikali ya Uingereza nchini Tanzania, Sally Hedley pamoja na wawakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) waliotembelea Mkoa wa Kagera kujionea hatua zilizochukuliwa ili kudhibiti ugonjwa huo. 


"Vile vile Serikali ilitoa elimu kwa jamii namna ya kujikinga na magonjwa ya mlipuko, kuimarisha huduma za dharura kwenye vituo vya afya na kuhakikisha uratibu mzuri kati ya Serikali na wadau wa maendeleo," amesema Dkt. Slyvanus


Kwa upande wake, Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) nchini Tanzania, Dkt. Alex Gsasira, ameipongeza Tanzania kwa hatua madhubuti zilizochukuliwa kudhibiti mlipuko huo, akisema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mzuri kati ya Serikali, wataalamu wa afya na wadau wa maendeleo.


Naye, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Dkt. Samwel Laizer, wakati wa ziara hiyo amesema ushiriki wa jamii katika kutoa taarifa za mapema, kufuata kanuni za afya na kushirikiana na wataalamu waliokuwa wakifuatilia wagonjwa uliwezesha kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo kwa haraka.


Mratibu wa Huduma za Afya Ngazi ya Jamii kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Norman Jonas, amesema wahudumu wa afya ngazi ya jamii walitoa mchango mkubwa kwa kutoa elimu ya afya nyumba kwa nyumba, jambo lililosaidia kuongeza uelewa na kuchangia kudhibiti maambukizi.