Ministry of Health

USALAMA WA MAJINI KUPEWA KIPAUMBELE KATIKA HUDUMA ZA CHANJO ZA MKOBA

Posted on: April 29th, 2026

Boti saba za kisasa zilizozinduliwa na Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, katika Bandari ya Nyamisati, zimetajwa kuwa na teknolojia ya hali ya juu inayolenga kuhakikisha usalama na kasi katika utoaji wa huduma za afya.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa boti hizo wilayaniRufiji Mkoani Pwani Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema Vyombo hivyo vimeundwa mahususi kuzingatia mazingira ya majini, vikiwa na vifaa vya kisasa vinavyowezesha watoa huduma kufika maeneo ya mbali kwa wakati.

Mhe. Mchengerwa amesema Kila boti imefungwa injini mbili zenye Horsepower 100 kila moja, jambo linaloipa boti uwezo mkubwa wa mwendo, uimara, na uhakika zaidi katika safari. Waziri alieleza kuwa hii ni hatua muhimu ya kuimarisha uwezo wa watoa huduma kufika kwenye maeneo yenye changamoto kubwa.

"Boti hizi ninazozindua leo zimetengenezwa kwa teknolojia ya kisasa inayozingatia ubora na usalama wa vyombo vya majini," alisema Mhe. Mchengerwa.

Pamoja na teknolojia ya injini, usalama wa abiria na watoa huduma umepewa kipaumbele kikubwa. Kila boti ina vifaa vya kujiokolea, ikiwemo life jackets nane, ili kuhakikisha usalama wakati wa safari. Waziri aliwataka watumiaji wa boti hizo kuzingatia kikamilifu kanuni za usalama majini na kutovuka uwezo wa abiria waliopangwa kwa kila chombo.

Mhe. Mchemherwa amesisitiza kuwa teknolojia bila nidhamu haitaleta ukombozi. Hivyo, aliwataka wahusika kuhakikisha kuwa boti hizi zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kwa kuzingatia taratibu zote za kisheria na usalama. Usimamizi mzuri wa teknolojia hii ndiyo njia pekee ya kuhakikisha kuwa uwekezaji huu unadumu na kuendelea kutoa huduma bora kwa jamii kwa muda mrefu.

Aidha, ameongeza kuwa boti hizo zitaongeza uwezo wa kutoa huduma za mkoba na tembezi kwa wakati, jambo ambalo ni muhimu katika utoaji wa chanjo. Hii itapunguza muda ambao watoa huduma wanatumia kusafiri na kuongeza muda wanaotumia kutoa huduma moja kwa moja kwa wananchi. Huu ni mfano mwingine wa jinsi Serikali inavyotumia teknolojia kuboresha huduma za umma.