Customer Feedback Centre

Ministry of Health

UONGOZI BORA UNAHITAJI NGUVU, UJASIRI, MAAMUZI NA KUSIKILIZA - WAZIRI UMMY

Posted on: April 6th, 2024



Na WAF - Dar Es Salaam 


Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema Ili kuwa kiongozi unahitaji kuwa na nguvu, ujasiri, usemi na msikilizaji, kwani kongozi unayogusa maisha ya watu kama yeye alivyokuwa Mama, Mbunge na Waziri ambapo pia alishawahi kushika nafasi nyingine ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI. 


Waziri Ummy amesema hayo leo Aprili 6, 2024 wakati wa ufunguzi wa mkutano wa uongozi wa wanawake katika Afya Duniani (WomenLift Health) uliofunguliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango katika ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar Es Salaam.


“Tunamshukuru Mungu kwa nchi yetu kupata heshima ya kuendesha mkutano huu mkubwa wa masuala ya uongozi wa wanawake katika Afya Duniani (WomenLift Health Grobal Conference) ambapo ni mara ya pili kufanyika Afrika”. Amesema Waziri Ummy 


Amesema, katika mkutano huo kuna ajenda kuu Tatu zitakazojadiliwa ambazo ni pamoja na uongozi wa mabadiliko, ushirikiano kama njia ya usawa wa kijinsia, na hatua za kuendeleza uongozi wa wanawake kwenye sekta ya Afya ambazo zinaendana vyema na uongozi wa mabadiliko wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. 


Aidha, Waziri Ummy amesema katika uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambae ni mwanamke na yeye kama Waziri wa Afya msaidizi wake, Tanzania imeweza kupunguza vifo vya kima mama wajawazito kwa zaidi ya asilimia 80 kutoka vifo 556 hadi vifo 104 katika kila vizazi hai laki 100,000.


“Lakini pia Tanzania imeweza kupunguza vifo vya watoto wenye umri chini ya Miaka Mitano kutoka vifo 67 katika kila vizazi hai Elfu 1,000 hadi vifo 43 katika kila vizazi hai Elfu 1,000, kwa sasa tunakwenda kuboresha huduma za Afya na kuhakikisha tunapunguza vifo vya watoto wachanga wenye umri wa siku 0-28”. Amesema Waziri Ummy 


Kwa upande wake Bi. Verda Msangi ambae ni mjumbe katika Mkutano huo amesema wapo tayari kujifunza kutoka kwa wanawake wengine ambao ni viongozi kwa kuwa bado wanawake wanaweza kuingia kwenye nafasi za uongozi wa juu katika Sekta ya Afya Kama Waziri wetu Mhe. Ummy Mwalimu. 



“Tupo hapa pia kujifunza na kuona jinsi gani tutashirikiana ili kuhakikisha Afya ya mwanamke na Afya za Watanzania zinaweza kuimarika kupitia mashirikiano hayo na mahusiano”. Amesema Bi. Msangi