Customer Feedback Centre

Ministry of Health

UJENZI WA HOSPITALI YA MBAGALA RANGI TATU, GHOROFA SITA ITAGHARIMU SH: BIL 10.8

Posted on: August 9th, 2023

Na. WAF - Dar es Salaam

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu leo ametembelea Hospitali ya Mbagala Rangi Tatu na kukagua mradi wa ujenzi wa hospitali hiyo itakayo kuwa na Ghorofa Sita na itagharimu shilingi Bilioni 10.8

Waziri Ummy amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameahidi kutoa Bilioni Mbili katika ujenzi wa jengo la ghorofa Sita la Hospitali ya Mbagala Rangi tatu ambalo litagharimu Bilioni 10.8 ili kupunguza changamoto za msongamano wa wagonjwa katika Hospitali hiyo iliopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Mkoani Dar es Salaam.

“Nilifanya ziara hapa mwaka juzi 2020 na mwaka jana 2021 nikapokea kero ya msongamano wa wagonjwa katika Hospitali hii na kuipeleka kwa Rais Dkt. Samia na ametoa Biloni Mbili ili kukamilisha ujenzi huu”, amesewa Waziri Ummy

“Baada ya Mhe. Rais Dkt. Samia kutoa Bilioni Mbili na Wizara ya Afya imetoa Bilioni Mbili pamoja na Halmashauri ya Manispaa ya Temeke wametenga Bilioni Mbili kwa hiyo tayari kuna Bilioni Sita, nimefanya kazi chini ya Rais Samia kwa karibu sana, fedha hizo zilizobakia ambayo ni Bilioni Nne ni ndogo chini ya uongozi wake”, amesema Waziri Ummy

Katika ziara hiyo Waziri Ummy amepokea taarifa ya hali ya maendeleo katika Sekta ya Afya ndani ya Wilaya ya Temeke Mkoani Dar es Salaam kutoka kwa Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe. Mobhare Matinyi.

Wakati akipokea taarifa kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Temeke Waziri Ummy amewataka watendaji wa Wilaya hiyo kuhakikisha wanatafuta maeneo ya kujenga majengo ya huduma za Afya ili kuwapunguzia wananchi changamoto ya msongamano wa kupata huduma.

Pia, Waziri Ummy amewaagiza watendaji hao kuhakikisha wanasimamia zoezi la kutoa chanjo kwa wasichana walio na umri wa miaka 14 ili waweze kujikinga na saratani ya mlango wa kizazi (HPV) ambapo kwa Mkoa wa Dar es Salaam wameweza kutoa chanjo hiyo kwa asilimia 106.

Mwisho, Waziri Ummy amesema Kwa sasa hali ya ujenzi wa jengo hilo ni asilimia Tano ambapo linatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 24, kwa fedha za Benki ya Dunia, Fedha za ndani ya Halmshauri na pamoja na fedha za Rais Samia.