Ministry of Health

UHAKIKI WA TAKWIMU ZA IPC WAIMARISHA USALAMA WA HUDUMA ZA AFYA

Posted on: March 13th, 2026

Na Abdu Iddy, Kigoma.


Wananchi wanaopata huduma katika vituo vya Kutolea huduma za afya wanatarajiwa kunufaika zaidi na ubora na usalama wa huduma kufuatia kuanza kwa zoezi la uhakiki wa ubora wa takwimu za Kukinga na Kudhibiti Maambukizo (IPC) pamoja na mafunzo kwa vitendo kwa watoa huduma za afya katika mikoa ya Kagera na Kigoma.


Zoezi hilo linafanywa na Wizara ya Afya (WAF) kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) pamoja na Shirika la CIHEB Tanzania chini ya mradi wa Usalama wa Afya Duniani, na linaendelea kuanzia Machi 10 hadi Machi 18, 2026 katika hospitali za rufaa za mikoa na hospitali za ngazi ya halmashauri pamoja na vituo vya afya vyenye wingi wa wagonjwa.


Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mratibu wa Zoezi hilo Dkt. Radenta Bahegwa amesema wataalam wa afya wanahakiki ubora wa takwimu zinazokusanywa na kutumwa katika mfumo wa taarifa za afya wa DHIS2 kuhusu viashiria 21 vya kukinga na kudhibiti maambukizo katika vituo vya kutolea huduma za afya.


“Uhakiki huo una lengo la kubaini hali halisi ya utekelezaji wa afua za kukinga na kudhibiti maambukizo ili kuwezesha maboresho ya huduma, hatua itakayosaidia kupunguza hatari ya maambukizo kwa wagonjwa, watoa huduma za afya pamoja na watu wanaofika katika vituo vya Kutolea huduma za afya kutafuta huduma,” amesema Dkt. Radenta.


Aidha, ameongeza kuwa sambamba na uhakiki huo, watoa huduma za afya wanapatiwa mafunzo kwa vitendo katika maeneo yao ya kazi ili kuwaongezea uwezo wa kufuatilia na kutekeleza kwa ufanisi viashiria vya IPC kwa kuzingatia miongozo ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kupitia vipengele nane muhimu vinavyoongoza programu za kukinga na kudhibiti maambukizo.


Kwa upande wake Muwakilishi kutoka Shirika la CIHEB Tanzania ambaye pia ni Meneja wa Tathmini nanUfuatiliaji Bi. Upendo Msanjila, amesema kuimarika kwa ukusanyaji na ufuatiliaji wa takwimu sahihi kutasaidia Serikali  na Wadau wake kupanga mikakati madhubuti ya kuboresha huduma za afya, hatua itakayochangia kuongeza usalama wa wagonjwa na ubora wa huduma zinazotolewa katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini.