Customer Feedback Centre

Ministry of Health

UCHUNGUZI WA UGONJWA WA UKOMA KUANZIA NGAZI YA KAYA

Posted on: January 28th, 2024

Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu amewataka Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri, kushirikiana na Vituo vyote vya kutolea huduma za Afya nchini kuhakikisha wanafanya uchunguzi wa Ugonjwa wa Ukoma kuanzia ngazi ya  kaya ili kupata wagonjwa wapya wa Ukoma na kutoa tiba kinga.


Prof. Nagu amesema hayo wakati akitoa tamko la Siku ya Ukoma Duniani Januari 28, 2024 Jijini Dodoma ambapo amesema 

Kila mwanajamii ana wajibu wa kutambua dalili za Ukoma na kuhakikisha wote wenye dalili wanafika katika kituo chochote cha kutolea huduma za afya kwa uchunguzi na matibabu.


"Nitoe rai kwa Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri, kushirikiana na Vituo vyote vya kutolea huduma za afya nchini kuhakikisha Kila Halmashauri nchini  inafanya juhudi kuibua wagonjwa, inafuatilia mwenendo wa ugonjwa, na kuwa na takwimu sahihi za kufuatilia wagonjwa kulingana na maeneo au vijiji au mitaa wanakopatikana". Amesema Prof. Nagu


Prof. Nagu ameongeza kuwa Idadi ya wagonjwa wapya imepungua kutoka wagonjwa 2,297 mwaka 2015 hadi wagonjwa 1,309 mwaka 2023 sawa na punguzo la asilimia 57. 


"Mwaka 2023 nchi yetu ilikuwa na wagonjwa 3 kwa kila watu 100,000 hivyo, Tanzania imefika kiwango cha awali cha shirika la Afya Duniani cha kutokomeza ugonjwa wa Ukoma yaani chini ya mgonjwa mmoja kati ya watu 10,000 tangu mwaka 2006" Amesema Prof Nagu


Prof. Nagu amesema Maadhimisho ya mwaka huu yamebeba kauli mbiu isemayo Thamini Utu; "Tokomeza Unyanyapaa dhidi ya Waathirika wa Ukoma". Ambapo amesema Kaulimbiu hiyo inachagiza umuhimu wa kila Mtanzania kushiriki katika kutokomeza ugonjwa huo

 

"Ugonjwa wa Ukoma si ugonjwa wa kulogwa, kurithi, wala laana, ni ugonjwa wa kuambukizwa, unatibika na kupona. Hivyo naisihi jamii kuachana kabisa na dhana hizo potofu na aina zote za unyanyapaa" amesema Prof Nagu.