Customer Feedback Centre

Ministry of Health

TUJIKINGE DHIDI YA KICHAA CHA MBWA

Posted on: September 29th, 2023


Na WAF - Dodoma


Wananchi wametakiwa kuwachanja wanyama wanaowafuga ili kujikinga na kupambana na ugonjwa wa Kichaa cha Mbwa.


Hayo yamebainishwa na Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Bw. Arbogast Waryoba, wakati wa maadhimisho ya ugonjwa wa kichaa cha mbwa duniani yaliyofanyika Wilaya ya Mpwapwa Mkoani Dodoma.


Aidha Waryoba amesisitiza kuwa ugonjwa wa kichaa cha mbwa unaathiri afya ya mtu kutokana na kuambukizwa na kirusi kitokanacho na wanyama jamii ya Paka, Mbwa, Mbweha, Fisi ambapo huambukizwa kwa kung’atwa na mnyama wenye ugonjwa huo.


“Pamoja na ugonjwa huu kusababisha vifo, ugonjwa huu umesababisha athari za kiuchumi kwa sababu ya gharama ya matibabu yake. Ugonjwa huu unakadiriwa kusababisha vifo 59,000 duniani”. Amesema Waryoba


Aidha Waryoba amesema kuwa serikali imeendelea kutekeleza juhudi za kudhibiti ugonjwa huu kwa kutoa elimu kwa umma, kuboresha utekelezaji wa dhana ya afya nchini, kurahisisha upatikanaji wa chanjo ya Kichaa cha Mbwa kwa wananchi, na chanjo kwa wanyama, hasa mbwa na paka,

Sambamba na hilo Waryoba amesema kuwa serikali inaendelea kutekeleza juhudi za kudhibiti na kupambana na ugonjwa huu kwa kuangalia namna ya kupunguza bei ya chanjo kwa wanyama.


Hata hivyo Waryoba amesema serikali imewezeshwa na shirika la usambazaji wa chanjo duniani kuridhia chanjo ya ugonjwa wa kichaa cha mbwa kuingizwa katika mfumo wa chanjo za kawaida, ambazo gharama zinatarajiwa kushuka zaidi pale taratibu za utekelezaji wa jambo hili utakapokamilika.


Aidha amesema kuwa katika kipindi hiki cha maadhimisho, jumla ya dozi 180,000 za chanjo ya Kichaa cha Mbwa zimesambazwa nchini kuanzia Septemba 24 mpaka 28, ambapo jumla ya mbwa 9,500 na paka 150 wamekwisha chanja.


Hata hivyo, juhudi za pamoja zinahitajika kwa sekta zinazohusika ili kuutokomeza ugonjwa huu. Kutokana na madhara ya ugonjwa huu kwani serikali imechukua jukumu la uchanjaji wa wanyama hao ikiwa ni sehemu ya upambanaji dhidi ya ugonjwa wa Kichaa cha Mbwa.