Customer Feedback Centre

Ministry of Health

TIBA ASILI KEMEENI VITENDO VYA UKATILI

Posted on: August 28th, 2024

Na WAF-MWANZA 


Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Saidi Mtanda amewataka watoa huduma za afya kwa njia ya tiba asili nchini kushirikiana na serikali kukemea na kutokomeza vitendo vya ukatili ndani ya jamii.


Mtanda ametoa kauli hiyo Agosti 28,2024 wakati akifungua Juma la Tiba asili na maadhimisho ya tiba asili kwa Mwafrika yanayofanyika kwenye viwanja vya Furahisha Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza.


"Ninyi Waganga wa Tiba asili mnamchango mkubwa katika kuimarisha afya za watanzania, hivyo tukiunganisha nguvu baina ya dawa zenu na zile za hospitalini wananchi watastawi kwakuwa na afya njema." Amesema Mhe. Mtanda na kuongeza


"Ni rai yangu, sisi wote tuungane kutokomeza vitendo vya ukatili wa mauwaji ya Albino na watoto ambayo yamekuwa yakiripotiwa hivi karibuni" amesisitiza Mtanda


Mkuu wa Mkoa Mtanda, ametumia fursa hiyo kuwataka waganga wa tiba asili wote kujisajili kwenye baraza la tiba asili na mbadala na kuhuisha leseni zao kila mwaka ili kuepuka kukumbwa na mkono sheria.


"Mimi ninaamini tiba hizi za asili zinapoboreshwa zinafanya kazi sawa na tiba hizi za kawaida na ndio maana Watanzania zaidi ya asilimia 60 nchini wanatumia tiba hizi na zinawasaidia, wote tunatambua kwamba tiba asili na tiba mbadala zimekuwa na mchango mkubwa kwa wananchi na ofisi ya mkuu wa mkoa kupitia idara ya afya "Amesema Mhe. mtanda


Kwa upande wake Mwenyekiti msaidizi baraza la tiba asili na mbadala nchini Dkt. Elizabeth Lema amesema waganga wa tiba hizo wametoka kwenye mfumo wa kufanya kazi zao kienyeji na sasa wanafanya kisasa na wakati mwengine wanatoa huduma jumuishi na wataalamu kutoka hospitali za kawaida ambao wanakiri kwamba tiba za asili zinamsaada mkubwa katika kutibu magonjwa mbalimbali.


Naye Msajiri wa baraza la tiba asili na mbadala Martin Mgogwa amebainisha kuwa baraza hilo pamoja na kuwasajiri linasimamia, kuthibiti na kuendeleza tiba asili nchini kwa kuhakikisha kila anayetoa huduma za tiba asili anasajiriwa pamoja na kuhuisha leseni kila mwaka katika eneo lake.


Akizungumza katika hafla hiyo ya ufunguzi Meneja wa Kanda ya ziwa wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia mkuu wa serikali ametoa wito kwa wadau kuhakikisha wanafika kwenye ofisi hizo ili dawa wanazotumia ziweze kuchunguzwa kama zina kemikali dawa badala ya kuwa na sumu.


Maadhimisho hayo ya tiba asilia ya Mwafrika yaliyoanza tangu Agosti 25 mpaka Agosti 31 yanalengo la kusimamia utoaji huduma bora na salama za tiba asili kupitia mifumo sahihi ya udhibiti.