Customer Feedback Centre

Ministry of Health

TANZANIA YAWEKEZA KUKABILIANA NA VIFO VITOKANAVYO NA MAGONJWA YA MOYO

Posted on: January 25th, 2025

Na WAF - Dar es Salaam

Serikali kupitia Wizara ya Afya imeendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya ili kukabiliana na vifo vitokananvyo na magonjwa ya moyo ambapo takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) za mwaka 2019 zinaonyesha kuwa, takriban watu milioni 17.9 hupoteza maisha kila mwaka kutokana na magonjwa hayo ikiwa ni sawa na asilimia 32 ya vifo vyote.

Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema hayo leo Januari 24, 2025 kwenye uzinduzi wa Kliniki ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo Oyster Bay Jijini Dar es Salaam.

"Kati ya vifo hivi, asilimia 85 husababishwa na mshtuko wa moyo pamoja na kiharusi, takwimu hizi zinaonyesha ukubwa wa tatizo la magonjwa haya Duniani na Tanzania ikiwemo," amesema Waziri Mhagama

Waziri Mhagama amesema kutokana na changamoto hiyo kubwa Duniani Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya uwekezaji mkubwa kwa kiwango cha kimataifa kwenye vifaa tiba pamoja na mitambo mbalimbali ikiwemo mashine za uchunguzi wa magonjwa kama MRI, CT- Scan pamoja na Ultrasound.

Aidha, Waziri Mhagama amesema kuwa Serikali imeendelea kuhakikisha Hospitali zinakuwa na uwezo wa kutoa huduma za matibabu kwa wananchi katika namna mbalimbali ikiwemo programu ya tiba mkoba (Outreach Programe) ijulikanayo kwa jina la Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach programe.

Katika hatua nyingine Waziri Mhagama amesema utekelezaji wa mkakati wa bima ya afya kwa wote unaendelea na huu unakwenda kuwa muarobaini wa changamoto nyingi za upatikanaji wa huduma za afya hapa nchini, "na kwa pamoja tuungane katika kuwaelimisha wananchi umuhimu wa Bima ya afya kwa wote kuwa ndio mkombozi wa huduma za matibabu kwa watanzania," amesema Waziri Mhagama

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Dkt. Kisenge amesema Taasisi hiyo wanaweza kuwaona wagonjwa hadi 300 wa upasuaji wa tundu na wagonjwa 800 wa upasuaji wa kifua kwa siku, ambapo wamejiwekea malengo ya kuwaona wagonjwa 3500 wa upasuaji wa tundu kwa mwaka na wagonjwa 900 wa upasuaji wa kifua kwa mwaka.