Customer Feedback Centre

Ministry of Health

TANZANIA NA AFRIKA KUSINI ZASAINI MAKUBALIANO YA USHIRIKIANO KATIKA SEKTA YA AFYA

Posted on: September 1st, 2023

Na WAF, Johanesburg - Africa Kusini


Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Afrika Kusini zimesaini hati ya makubaliano katika Sekta ya Afya. 


Makubaliano hayo yamesainiwa leo Septemba 1, 2023 na Waziri wa Afya Tanzania Mhe. Ummy Mwalimu pamoja na Waziri wa Afya wa Afika Kusini Mhe. Dkt. Mathume Joseph Phaahla mjini Johannesburg, Afrika Kusini.


“Tanzania na Afrika Kusini tumekuwa na ushirikiano wa muda mrefu katika Sekta mbalimbali ikiwemo Sekta ya Afya, hivyo tumesaini makubaliano hay ambayo yataenda kuchangia na kuboresha ushirikiano ikiwemo kubadilishana wataalam wabobezi kwenye fani mbalimbali za Afya”, amesema Waziri Ummy 


Pia, Waziri Ummy amesema makubaliano hayo yataenda kuwezesha mafunzo ya muda mfupi na muda mrefu na kubadilishana teknolojia, kuboresha upatikanaji wa dawa, chanjo na udhibiti wa magonjwa ya mlipuko pamoja na dharura za Afya.


“Laini pia, tutaweza kuimarisha mfumo wa huduma za rufaa kwa wagonjwa watakaohitaji matibabu nchini Afrika Kusini”, amesema Waziri Ummy


Aidha, Waziri Ummy amesema kuwa kusainiwa kwa hati hiyo, ni moja ya maazimio ya Mkutano wa Pili wa mataifa mawili (Bi - National Commission - BNC) baina ya Tanzania na Afrika Kusini.


“Azimio namba 43 lilielekeza kwamba, hati ya Makubaliano katika Sekta ya Afya isainiwe baada ya taratibu zote ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini Mhe. Cyril Ramaphosa”, amesema Waziri Ummy 


Amesema, Katika hati hiyo viongozi hao wawili walisisitiza umuhimu wa kutekeleza maafikiano yaliyofikiwa na kutoa mrejesho wa utekelezaji kwa wakati. 


Kwa upande wake Waziri wa Afya wa Afrika Kusini Mhe. Dkt. Phaahla amepongeza hatua ya kusainiwa kwa hati ya makubaliano hayo ambayo yamefanyika katika kipindi ambacho nchi za Dunia nzima na Bara la Afrika zikiwemo nchi za Afrika Kusini na Tanzania zinakabiliwa na majanga mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya tabia nchi inayopelekea milipuko ya magonjwa mbalimbali na ukosefu wa vyakula.


“Utiaji saini huu wa makubaliano haya utaimarisha zaidi ushirikiano katika masuala yaliyoanzishwa kama vituo vya kudhibiti na kuzuia magonjwa, wakala wa dawa, mifumo ya ununuzi wa pamoja wa dawa”, amesema Waziri Dkt. Phaahla


Mwisho, Mawaziri wote wawili kwa pamoja wamekubaliana kuwa na mpango wa utekelezaji na ufuatiliaji wa mkataba huo utatolewa taarifa kila Mwaka.