Customer Feedback Centre

Ministry of Health

TANZANIA KUSIMAMIA MATUMIZI SALAMA YA KEMIKALI NA TAKA ZA KEMIKALI

Posted on: September 29th, 2023

 Na. WAF - Bonn, Ujerumani


Serikali ya Tanzania kupitia wizara ya Afya imesisitiza kuendelea kusimamia matumizi salama ya Kemikali na taka zitokanazo na Kemikali ili kuzuia athari kwa  wananchi.


Hayo yamebainishwa leo Septemba 29, 2023 na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe wakati akiwasilisha tamko la Tanzania katika Mkutano wa tano wa Kimataifa wa Usimamizi wa matumizi salama ya Kemikali Duniani (ICCM5) kwa niaba ya Mhe Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu.


Aidha, Dkt Magembe alieleza kuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe Rais, Dkt Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuchukua hatua madhubuti kudhibiti matumizi mabaya ya Kemikali ili kuhakikisha usalama wa wananchi na mazingira nchini kwa kutekeleza kwa vitendo malengo endelevu ya maendeleo ya Dunia na katika kujenga uchumi endelevu wa nchi. 


“Pamoja na kuwa matumizi ya Kemikali  ni muhimu na zipo faida nyingi zitokanazo na kemikali hasa katika sekta za Afya, Kilimo, Elimu, Viwanda nk, shughuli za kemikali zisiposimamiwa vizuri, zinaweza kuwa na athari kubwa kwa afya ya binadamu,  mazingira, usalama mahala pa kazi, ulinzi na usalama wa nchi”. Amesema Dkt. Magembe 


Pia Dkt. Magembe amesema kuwa takwimu za Shirika la Afya Duniani zinaonyesha, takribani vifo milioni mbili duniani  kwa mwaka vinatokana na matumizi mabaya ya Kemikali yakiwemo madhara mengine kama ulemavu, kuharibika kwa mimba, magonjwa ya mfumo wa hewa na saratani. 


Sambamba na hilo Dkt. Magembe amebainisha mipango ya Tanzania katika matumizi ya kemikali hizo ikiwa ni Pamoja na kuimarisha uratibu na usimamizi wa Kemikali ndani ya nchi Pamoja na kutenga rasilimali za kutosha ikiwemo fedha ili kuwezesha utekelezaji wa mpango mkakati huo, hususani kuziwezesha nchi zinazoendelea kuzuia na kudhibiti madhara yatokanyo na matumizi ya Kemikali.


Aidha Dkt. Magembe ameziomba nchi zilizoendelea kushirikiana na nchi zinazoendelea katika kuwekeza kwenye teknolojia za kisasa kwenye viwanda vinavyozalisha dawa, vifaa tiba, mbolea, viuatilifu  na bidhaa nyinginezo kwa lengo la kuzalisha bidhaa rafiki kwa afya ya binadamu na mazingira na pia kudhibiti taka zitokanazo na bidhaa hizo.