Customer Feedback Centre

Ministry of Health

TANZANIA, GLOBAL FUND KUENDELEZA USHIRIKIANO KUIMARISHA AFUA ZA MALARIA, TB NA UKIMWI

Posted on: July 1st, 2025

NA WAF - Dodoma 


Serikali kupitia Wizara ya Afya na Global Fund kuendelea kushirikiana ili kuimarisha afua dhidi ya Malaria, Kifua Kikuu (TB) pamoja na UKIMWI kwa kuboresha huduma za afya na upatikanaji wa dawa, vifaa na vifaa tiba.


Waziri wa afya Mhe. Jenista Mhagama amesema hayo leo Julai 01, 2025 alipokutana na Mkuu wa Idara ya usimamizi wa ruzuku kutoka Mfuko wa Kimataifa (Global Fund) Bw. Edwin Edington katika ofisini za wizara Jijini Dodoma.


Waziri Mhagama amesema mazungumzo hayo yamelenga kujadili masuala mbalimbali yanayohusu sekta ya afya nchini kwa lengo la kutekeleza malengo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora ya afya katika maeneo yao. 


"Serikali ya Tanzania itaendelea kushirikiana na mfuko huu kwakuwa umekuwa na mchango mkubwa katika kuwezesha bidhaa za afya ikiwemo dawa, vifaa na vifaa tiba kama ilivyo azima ya Serikali ya awamu ya Sita (6) ya kujenga miundombinu na kuboresha masuala ya tiba kwa wananchi," amesema Waziri Mhagama 


Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya usimamizi wa Ruzuku Bw. Mark Edington kutoka Mfuko wa Kimataifa wa kusaidia mapambano dhidi ya  UKIMWI, TB na Malaria (GLOBAL FUND) ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na mfuko huo katika kupiga vita maradhi ya Kifua Kikuu, Malaria na Ukimwi.


Bw. Edington ameahidi kuwa Mfuko wa Dunia utaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali za kukabiliana na magonjwa hayo hapa nchini kwa kuelekeza rasilimali fedha kwa ajili ya kununua dawa pamoja na kuboresha mifumo ya utoaji huduma ya afya.


Katika kikao hicho pia kimehudhuriwa na timu kutoka Wizara ya Afya ikiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekaaghe pamoja na Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe.