Customer Feedback Centre

Ministry of Health

TAASISI YA SASAKAWA HEALTH FOUNDATION YA JAPAN YAAHIDI KUSHIRIKIANA NA TANZANIA KATIKA KUTOKOMEZA UGONJWA WA UKOMA NCHINI

Posted on: September 29th, 2023

Na. WAF Dar es Salaam


Taasisi ya Sasakawa Health Foundation chini ya Mwavuli wa Taasisi Mama ya The Nippon Foundation ya Nchini Japan wameahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kutokomeza ugonjwa wa Ukoma kabla ya Mwaka 2030. 


Hayo yamejiri leo Septemba 29, 2023 wakati wa kikao kifupi kati ya Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu (Mb) na Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Sasakawa Health Foundation Prof. Takahiro Nanri kilichofanyika katika ofisi ndogo za Wizara ya Afya Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Balozi wa Japan nchini Tanzania, Mhe. Yasushi Misawa.


Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amewakarabisha na kumshukuru Mhe. Balozi Misawa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo kwa kuonyesha nia ya dhati katika kupambana na Ugonjwa wa Ukoma ambao umegubikwa na sifa ya unyanyapaa na kutengwa kwa wanaoathirwa na ugonjwa huo.


Aidha, Waziri Ummy amesema kuwa bado ugonjwa wa UKOMA upo nchini na Tanzania ni moja ya nchi 23 zilizobainishwa na WHO kuwa ni za kipaumbele katika kutokomeza ugonjwa wa UKOMA. Alieleza kuwa dawa za kutibu ugonjwa huu zipo na huduma zinatolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan bila malipo kwa wagonjwa wote wenye Ukoma na mgonjwa anapona kabisa.


“Kwa kuendelea kushirikiana kwa pamoja na kuangalia maeneo ya ushirikiano tunaweza kutokomeza kabisa ugonjwa wa Ukoma ifikapo Mwaka 2030”. Amesema Waziri Ummy


Balozi Misawa amesema lengo la ziara hiyo ni kuja kuleta salaam kutoka kwa Balozi wa Dunia Mhe. Yohei Sasakawa katika kutokomeza ugonjwa wa Ukoma Duniani ikiwa ni pamoja na kuonyesha nia ya kuja nchini kupanda Mlima Kilimanjaro na kuweka bendera juu ya kilele cha Bara la Afrika ili kuhamashisha mataifa yote kuongeza kasi ya kutokomeza Ukoma barani Afrika kabla ya Mwaka 2030.


Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sasakawa Health Foundation Prof. Takahiro Nanri ameelezea namna ambavyo Serikali ya Japan kupitia Taasisi hiyo itakavyoweza kusaidia kutekeleza mpango wa Wizara wa kutokomeza kabisa Ukoma na madhira yake ifikapo mwaka 2030.