Customer Feedback Centre

Ministry of Health

TAASISI YA LV PRASAD YA MACHO NCHINI INDIA KUSHIRIKIANA NA WIZARA YA AFYA KATIKA KUIMARISHA HUDUMA ZA MACHO

Posted on: July 29th, 2023

Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Taasisi ya Huduma za Macho ya LV Prasad iliyopo mjini Hyderabad wataandaa Hati ya mashirikiano (MoU) yenye lengo la kuimarisha huduma za macho nchini Tanzania.

Hayo yamebainishwa leo na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu leo tarehe 30.07.23 alipotembelea Taasisi ya Huduma za Macho ya LV Prasad iliyopo mjini Hyderabad nchini India

Waziri Ummy ameeleza kuwa lengo la Hati ya mashirikiano hayo ni kuhakikisha huduma za kibingwa za macho ikiwemo kurudisha uoni (Vision Rehabilitation), uchunguzi na matibabu ya Magonjwa mbalimbali ya macho ili wananchi wanufaike na Huduma hizo.

“Taasi hii ina jumla ya vituo vya kutolea huduma vipatavyo 275 nchini India, Hospitali hii inatoa huduma kwa malipo lakini pia sera ya Hospitali ni kutoa huduma kwa msamaha hadi kufikia asilimia 50 ya wapokea Huduma”, ameeleza Waziri Ummy.

Aidha Waziri Ummy amesema kwa mujibu wa takwimu za Taasisi hiyo ni kwamba, imeweza kuhudumia wagonjwa milioni 36.89 tangu kuanzishwa kwake, Huduma zinazotolewa ni pamoja na kurudisha uoni ( Vision Rehabilitation), uchunguzi na matibabu ya Magonjwa mbalimbali ya macho.

Taasisi hiyo inayo matawi yake yanayojihusisha zaidi na Huduma za matibabu, Mafunzo, Taasisi ya Macho pamoja na Taasisi inayojihusisha na utoaji wa huduma ngazi ya jamii.

Vile vile Waziri Ummy ameishukuru Taasisi hiyo kwa kuendelea kushirikiana kwa karibu na Tanzania ikiwemo kutoa huduma za kambi za matibabu nchini Tanzania

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi Dkt. Gullapalli Rao, ameahidi kusaidia mtaala wa mafunzo utakaotumiwa na watoa huduma ngazi ya jamii ili wapate uelewa wa huduma za macho.
“Elimu hiyo itawasaidia watoa Huduma ngazi ya Jamii kugundua maradhi ya macho kwenye jamii na kuhamasisha wagonjwa kuwahi katika vituo vya kutolea Huduma za afya”, ameeleza Dkt. Rao

Hata hivyo, Dkt. Rao ameahidi kuwa, Taasisi itashirikiana na Hospitali za Tanzania katika kutoa mafunzo ya ubobezi kwa wataalam ili kuboresha huduma za macho nchini.