Customer Feedback Centre

Ministry of Health

TAARIFA ZA VIFO VITOKANAVYO NA UZAZI ZITOLEWE, KUSAIDIA MABORESHO.

Posted on: August 21st, 2024

Na WAF – Mtwara


Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara Ndg. Abdillah Mfinanga ametoa agizo kwa wahudumu wa Afya Kanda ya Kusini kutoa taarifa zote za vifo vya mama na mtoto ikiwa pamoja na sababu ya vifo hivyo ili kusaidia namna ya kufanya maboresho kwenye huduma ya mama na mtoto.


Ndg. Mfinanga ameyasema hayo leo Agosti 21, 2024 katika ukumbi wa Boma uliopo ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, akiwa amemuwakilisha Katibu Tawala mkoa wa Mtwara wakati akifungua kikao cha siku mbili cha tathmini ya huduma za Afya ya uzazi, mtoto na vijana kanda ya kusini ili kufanya maboresho na kutoa huduma za Afya kwa ufanisi zaidi.


Amesema utoaji wa taarifa hizo itasaidia Serikali kujua ilipo changamoto na kuitatua kwa lengo la kuendelea kupunguza vifo vitokanavyo na Uzazi, mama na mtoto kupitia juhudi za uwekezaji wa serikila kwenye kuboresha huduma za mama na mtoto.


Mfinanga amesema vikao vya ndani vifanyike kupata tathimini ya vifo vya mama na mtoto na kutoa nafasi kubwa kujadili vifo vya watoto. 


“kila Halmashauri ifanye vikao vya ndani na kutoa suluhu ya nini kifanyike kulingana na sababu mbalimbali ya vifo vilivyotokana na uzazi na vifo vya watoto wachanga pia taarifa hizo na utekelezaji wa maazimio itumwe ngazi ya Mkoa kila mwezi.” Amesema Mfinanga


Aidha, Ameongeza kuwa watu wanaohusika na ukusanyaji damu wa kila Halmashauri waongeze bajeti ili iweze kusaidia upatiknaji wa damu kwa wingi kwaajili ya kusaidi wakina mama wanao pungukiwa damu wakati wa kujifungua.


Kwa upande wake Bi. Faraja Mgeni, Afisa Programu Uzazi Salama akimuwakilisha Mkurugenzi Idara ya Afya ya Uzazi,Mama na Mtoto ameelezea malengo ya mkutano huo wa siku mbii wa kufanya tathmini ya huduma za Afya ya Uzazi,mtoto na vijana  Kanda ya Kusini.


“Malengo ya mkutano huu ni kupokea taarifa ya hali ya Afya ya Uzazi na Mtoto Ngazi ya Kanda na Mikoa yake, kujadii utatuzi wa changamoto zilizotokana na wasilisho la kila Mkoa, Kuandaa mpango kazi wa mwaka mmoja (kila Mkoa, kila Halmashauri) unaolenga kupunguza Vifo vinavyotokana na uzazi, watoto wanaozaliwa wafu na vifo vya watoto wachanga.” Amesema Bi. Mgeni.