Customer Feedback Centre

Ministry of Health

SHIRIKIANENI KATIKA UTOAJI WA HUDUMA BORA ZA AFYA ILI KUKABILIANA NA MAGONJWA YA MLIPUKO

Posted on: August 21st, 2024

Na WAF - Tunduma, Songwe


Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, amewataka watumishi wa afya kushirikiana kwa karibu katika utoaji wa huduma za afya ili kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi. 


Dkt. Mollel ametoa wito huo Leo Agosti 22, 2024 alipokuwa akitembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Songwe leo, ambapo amefanya ziara ya kukagua hali ya utoaji wa huduma na utayari wa hospitali hiyo katika kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.


Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Dkt. Mollel amesisitiza kuwa ushirikiano miongoni mwa watumishi ni msingi wa utoaji wa huduma bora kwa wananchi huku  akisisitiza kuwa, kila mtumishi anapaswa kushiriki kikamilifu katika majukumu yake na kufanya kazi kwa kushirikiana na wengine ili kuongeza ufanisi katika huduma zinazotolewa.


"Shirikianeni katika kutoa huduma za afya, kufanya kwenu vizuri kunaletwa na ushirikiano mlionao, mkiwa kitu kimoja ni rahisi kutoa huduma kwa pamoja," Amesema Dkt. Mollel.


Aidha, Dkt. Mollel ameeleza kuwa Serikali imewekeza katika miundombinu na vifaa vya kutosha kwa lengo la kuboresha huduma za afya, na hivyo akawataka watumishi kufanya kazi kwa weledi mkubwa ili kuhakikisha malengo hayo yanafikiwa.


Pia, Dkt. Mollel ameipongeza Menejimenti ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Songwe kwa usimamizi mzuri wa hospitali hiyo na akatoa rai kwao kuendelea kuchapa kazi kwa bidii.


Ziara ya Dkt. Mollel katika hospitali hiyo imekuja wakati ambapo Serikali inaendelea na juhudi zake za kukabiliana na magonjwa ya mlipuko pamoja na kuboresha huduma za afya nchini, hususan katika maeneo ya pembezoni