Customer Feedback Centre

Ministry of Health

SH. BILIONI 3 YATENGWA KUONGEZA MAJENGO HOSPITALI YA RUFAA KANDA YA KUSINI- MTWARA

Posted on: July 9th, 2023

Hayo yamesemwa Leo tarehe 07/07/2023 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa wakati akizungumza na Watumishi pamoja na wananchi wa Mtwara alipokuwa katika ziara yake ya kikazi katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Kusini.

Waziri Majaliwa amesema kuwa Serikali inaendelea kuboresha na kuongeza majengo ya kutolea huduma katika Hospitali hiyo ambapo kwa mwaka wa fedha 2023/2024 imetenga kiasi cha fedha Bilioni 3 ujenzi wa jengo la mama na mtoto, nyumba za Watumishi, jengo la kufulia pamoja na kichomea taka.

Mhe. Waziri Majaliwa ametoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa katika hospitali hiyo kutokana na uwepo wa majengo mazuri, vifaa tiba vya kisasa kama vile MRI, CT SCAN pamoja na huduma bora na nzuri zinazotolewa.

Waziri Majaliwa ameridhishwa na huduma zinazotolewa hospitalini hapo na hii inakuja baada ya Mhe. Waziri Majaliwa alipojiridhisha kupitia maoni ya wagonjwa waliokuja kutibiwa ambao wameeleza kuwa wanapata huduma nzuri huku wakitoa pongezi kwa Watumishi Kutokana na umahiri wao katika kazi lakini pia kuwa na lugha nzuri kwa wagonjwa wao.

Aidha Mhe. Waziri Majaliwa ameeleza kuwa Serikali imejenga Hospitali hiyo ili iwe mkombozi kwa wananchi wa Ukanda wa Kusini pamoja na nchi za jirani kama vile Msumbiji, Malawi na Visiwa vya Komoro hali itakayosaidia kupunguza gharama za kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za Afya.

Sambamba na hilo, Waziri Majaliwa amesema kuwa serikali inaendelea kufanya juhudi za kuhakikisha inaajiri watumishi waliobobea hospitalini humo ili iendelee kuwa kinara wa utoaji huduma bora kanda ya kusini na nchini pia.