Customer Feedback Centre

Ministry of Health

SERIKALI YATENGA BILIONI 1 UJENZI JENGO LA KUHIFADHIA MAITI MAWENZI

Posted on: November 27th, 2025

Na WAF - Kilimanjaro

Serikali imetenga Shilingi Bilioni 1 kwa ajili ya ujenzi wa jengo jipya la kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mawenzi, hatua inayolenga kuboresha huduma na kuondoa changamoto ya jengo la zamani lenye uwezo wa kuhifadhi miili 18 pekee.

Akizungumza leo Novemba 26, 2025 wakati wa ziara ya kukagua miradi ya maendeleo mkoani Kilimanjaro, Naibu Waziri wa Afya Dkt. Florence Samizi amesema hatua hiyo ni sehemu ya mpango wa Serikali kuboresha huduma za afya kwa ngazi zote.

Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, ameagiza ujenzi huo kuanza mara moja, akisisitiza umuhimu wa hospitali hiyo kuwa na miundombinu ya kisasa ili kuhudumia wananchi kwa ufanisi.

“Ujenzi huu uanze haraka ili tuondokane na mazingira duni ya zamani. Wananchi wanastahili huduma zenye heshima na hadhi,” amesema Dkt. Samizi.

Naibu Waziri ameagiza kukamilishwa kwa sehemu zilizobaki kwenye jengo la afya ya mama na mtoto, akibainisha kuwa licha ya ghorofa mbili kuwa zinatumika pia linapaswa kuanza kutumika kwa ghorofa zote ili kuongeza uwezo wa hospitali kutoa huduma muhimu.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri amewataka watumishi wa afya kufanya kazi kwa weledi, uadilifu na ari, sambamba na dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita kuboresha huduma za afya nchini.

Ziara hiyo imehusisha ukaguzi wa miradi mbalimbali ya uboreshaji wa miundombinu ya hospitali, ikiwemo majengo mapya yanayoendelea kujengwa chini ya utekelezaji wa mpango wa maendeleo wa Wizara ya Afya.