Customer Feedback Centre

Ministry of Health

SERIKALI YAPOKEA VIFAA VYA THAMANI YA TSH. MILIONI 569.7 KWA AJILI YA HUDUMA ZA SARATANI YA MATITI

Posted on: July 29th, 2025

Na WAF – Dar es Salaam


Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe amepokea vifaa tiba kwa ajili ya huduma za saratani ya matiti vyenye thamani ya Shilingi Milioni 569.7 kutoka shirika la Jhpiego Tanzania kupitia mradi wake wa BEAT Breast Cancer.


Makabidhiano hayo yamefanyika Julai 29, 2025 katika ofisi ndogo za Wizara ya Afya jijini Dar es Salaam, ambapo Dkt. Shekalaghe amesema vifaa hivyo vitasaidia kubaini saratani ya matiti katika hatua za awali na kuanza matibabu mapema, hatua itakayosaidia kupunguza vifo vinavyotokana na ugonjwa huo.


Ameeleza kuwa vifaa vilivyopokelewa ni pamoja na mashine 31 za ultrasound, sindano zaidi ya 10,000 za vipimo vya saratani ya matiti, pamoja na meza 31 za kubebea mashine hizo. Vifaa hivyo vitasambazwa katika mikoa yenye uhitaji mkubwa na idadi kubwa ya wanawake waliothirika na ugonjwa huo ikiwemo Mtwara, Morogoro na Tanga.


“Jumla ya thamani ya vifaa hivi tunavyopokea leo ni takribani Shilingi Milioni 569.7. Tunaamini vitakwenda kuokoa maisha ya watu wengi, hususan wanawake,” amesema Dkt. Shekalaghe.


Aidha, ametoa pongezi na shukrani kwa Shirika la Jhpiego kwa kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania, hasa katika kipindi hiki ambacho dunia inakabiliwa na changamoto mbalimbali za kiuchumi.


Mradi wa BEAT Breast Cancer unatekelezwa kwa ufadhili wa Pfizer Foundation, kwa ushirikiano wa karibu na Wizara ya Afya pamoja na Ofisi ya Rais TAMISEMI.