Ministry of Health

SERIKALI YAIMARISHA ULINZI HOSPITALINI DHIDI YA MAAMBUKIZI KUPITIA UZALISHAJI WATAALAM BINGWA WA NDANI

Posted on: April 27th, 2026

Na Cletus Sanga – WAF, Morogoro

Serikali kwa kushirikiana na Shirika la CIHEB Tanzania kupitia mradi wa Usalama wa Afya Duniani (Global Health Security), imeendelea kujenga mtandao imara wa wataalamu wakufunzi (ToTs) wanaosaidia kudhibiti maambukizi katika vituo vya kutolea huduma za afya.

Hayo yamebainishwa leo Aprili 27, 2026, Mkoani Morogoro na Mkuu wa Kitengo cha Kuzuia na Kudhibiti Maambukizi Kitaifa, Dkt. Joseph Hokoro wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha kuandaa orodha ya vifaa muhimu vya Kinga na Udhibiti wa Maambukizi (IPC Catalogue), kukamilisha uchambuzi wa takwimu pamoja na kuongeza viashiria vipya katika mfumo wa DHIS2.

Dkt. Hokororo amesema kupitia mradi wa Usalama wa Afya Duniani, hospitali za rufaa za mikoa na wilaya zimeendelea kuwa na wataalamu wenye uwezo wa kusimamia mbinu bora za Kinga na Udhibiti wa Maambukizi bila kutegemea wataalamu wa nje kila wakati.

“Uwekezaji huu katika rasilimali watu kupitia mradi wa Usalama wa Afya Duniani ndiyo uti wa mgongo wa usalama wa afya. Tunapokuwa na wakufunzi wengi wa ndani, tunakuwa na uhakika wa uendelevu wa huduma bora kwa wananchi wetu, na hiyo ndiyo dhamira ya Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan. Mafunzo haya yamejenga uwezo wa kudumu kwa watumishi wetu na kutuwezesha kukabiliana kwa haraka na kwa ufanisi katika kupambana na kudhibiti milipuko ya magonjwa,” amesema Dkt. Hokororo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mradi wa Usalama wa Afya Duniani kutoka CIHEB Tanzania, Dkt. Edgar Lusaya, amesema katika robo ya pili ya mwaka huu mradi huo unaendelea kutekeleza mafunzo mbalimbali ya kiufundi kwa watumishi wa afya katika mikoa tofauti nchini.

Amesema kwa upande wa Zanzibar, wataalamu 31 wanapatiwa mafunzo ya ngazi ya kati na ya juu ili kuunda kundi la wakufunzi watakaosaidia kuimarisha huduma za afya visiwani humo.

Dkt. Lusaya ameongeza kuwa mkoa wa Lindi pia umeendelea kunufaika na mradi huo ambapo wataalamu 38 wanapatiwa mafunzo ya kuimarisha utekelezaji wa Kinga na Udhibiti wa Maambukizi kwa kutumia zana za kidijitali za usimamizi wa usafi.