Customer Feedback Centre

Ministry of Health

SERIKALI YABAINISHA VIPAUMBELE 6 VYA KISERA KATIKA SEKTA YA AFYA 2024/25

Posted on: February 15th, 2024


Na. WAF - Dodoma

Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo imebainisha vipaumbele Sita vya kisera katika Sekta ya Afya ambavyo vitawekewa mkazo zaidi katika kutekelezwa kwa mwaka 2024/25 ili kuendelea kuboresha huduma za Afya nchini.

Waziri wa afya Mhe. Ummy Mwalimu amebainisha hayo leo Februari 15, 2024 kwenye Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Kisera wa 23 wa Sekta ya Afya uliofanyika Jijini Dodoma ambapo amesisitiza kipaumbele cha kwanza kuwa ni rasilimali watu katika Afya.

“Serikali imejitolea kuwekeza katika mafunzo na maendeleo ya watumishi wa Afya ili kuhakikisha huduma bora zinapatikana kwa wananchi.” Amesema Waziri Ummy

Waziri Ummy amebainisha vipaumbele hivyo ambavyo ni pamoja na Rasilimali watu katika Afya, swala la ubora wa huduma za Afya, utekelezaji wa sheria ya Bima ya Afya kwa wote, wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii, mapambano dhidi ya Magonjwa Yasiyoambukiza na Kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na Sekta binafsi katika utoaji huduma za Afya.

“Suala la ubora wa huduma za Afya tunaendelea kulisisitiza kwa kuzingatia umuhimu wa kuboresha huduma kwa wateja pamoja na kuhakikisha usalama wao ili mteja apate huduma iliyokua nzuri.” Amesema Waziri Ummy

Aidha, katika vipaumbele hivyo Waziri Ummy ametaja utekelezaji wa sheria ya bima ya Afya kwa wote kuwa ni moja ya vipaumbele vya Serikali katika kuhakikisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wote ambapo sheria ya Bima ya Afya kwa wote imeshasainiwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Sasa ni utekeleaji wake.

Waziri Ummy ameelezea juhudi za Serikali katika kuhudumia jamii na kuimarisha huduma za afya ngazi ya jamii, umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na wadau wengine huku akiongeza kwakusema kuwa Serikali inaongeza nguvu katika mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza kwa kutoa elimu kwa umma na kuboresha huduma za tiba.

Pia, Waziri Ummy amehimiza umuhimu wa kuzungumzia masuala ya afya ya akili na ajali, na kusisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na sekta nyingine katika kuhakikisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wote.