Customer Feedback Centre

Ministry of Health

SERIKALI, WADAU WAJIPANGA KUTOKOMEZA FISTULA IFIKAPO 2030

Posted on: May 23rd, 2024



Na WAF, ARUSHA

Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa ushirikiano na asasi za kiraia imejiwekea malengo ya kutokomeza maradhi ya Fistula yatokanayo na uzazi pingamizi ifikapo 2030 ikiwa ni miaka sita kutoka hivi sasa.

Jitihada hizo, zitakwenda sambamba na kuongeza elimu miongoni mwa jamii, kuachana na mila potofu lakini pia kuwahimiza wazazi kuwahi kliniki pindi wapatapo ujauzito ili kuepuka uzazi pingamizi.

Akihutubia katika Kilele cha Siku ya Fistula Duniani akiwa Mgeni Rasmi kwa Mualiko wa Waziri wa Afya, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima Mei 23, 2024 jijini Arusha yenye Kaulimbiu isemayo.‘Vunja mnyororo: Zuia fistula ya uzazi Tanzania, amesema dhamira ya Serikali nikuona maradhi hayo yanafikia ukomo.

"Kama taifa tumezatiti kuhakikisha tunatokomeza Fistula ndani ya miaka sita ijayo, lakini jitihada hizi haziwezi kufanikiwa bila kuwa na nguvu za pamoja na wadau wetu asasi za kiraiya. Lakini pia jamii kwa ujumla" amesema Dkt. Gwajima na kuongeza.

"Upo umuhimu wa jamii kuwahimiza wajawazito kuanza kliniki mapema, na hasa mimba ikiwa na umri chini ya wiki 12, lakini pia kuhudhuria mahudhurio angalau manne mpaka mama anapofikia kipindi cha kujifungua", amesisitiza Dkt. Gwajima

Katika hatua nyingine Dkt. Gwajima amesema, takwimu za wajawazito waliohudhuiria Kliniki mapema kwa kipindi cha Julai 2023 hadi Machi 2024, zinnaonyesha waliofikia mahudhurio manne au zaidi walikuwa 2,208,391 sawa na asilimia 119.5 ya waliotarajiwa.

Akitoa salam za Wizara ya Afya Dkt. Mwinyi Kondo Mkurugenzi Msaidizi wa Idara huduma za wazee na utengemao amesema serikali imeendelea kuboresha huduma za afya.

"Kuongezeka kwa bajeti ya Serika kutoka Trilion 1.2 kwa mwaka 2023/24 hadi Trilioni 1.3 kwa mwaka huu wa 2024/25 ni dhahiri kwamba Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuboresha huduma za afya ikiwepo suala la uzazi" amesema Dkt. Mwinyi.