Customer Feedback Centre

Ministry of Health

SERIKALI KUTOA MAFUNZO KWA WAHUDUMU WA AFYA ILI KUBORESHA HUDUMA

Posted on: July 26th, 2023

Serikali kwa kushirikiana na shirika la MUSO Health imepanga kuimarisha mifumo ya kutolea huduma za afya ngazi ya jamii.

Hayo yamebainishwa na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu mapema leo Julai 27, 2023 ambapo alikutana na ujumbe kutoka shirika la MUSO Health katika kikao cha pamoja kilichofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Afya Jijini Dodoma.

Prof. Nagu amesema Serikali ina mkakati wa kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wa huduma za Afya kwenye jamii ili kuboresha utolewaji wa huduma za Afya ngazi ya jamii nchini.

"Mafunzo haya yatadumu kwa muda wa miezi sita kwa ajili ya kuwajengea uwezo watoa huduma katika vituo vya Afya ngazi ya Jamii kutoa huduma bora kwa wananchi ili kupunguza kasi ya magonjwa yanayoambukiza na yasiyoambukiza". Amesema Prof. Nagu.

Aidha, Prof. Nagu amewapongeza Shirika la MUSO Health kwa jitihada wanazofanya katika kuimarisha mifumo ya kutolea huduma za afya katika ngazi ya jamii kwani ni fursa ya kujifunza mifumo mizuri ya uboreshaji huduma za afya ngazi ya jamii.

Kwa upande wake mwakilishi wa MUSO HEALTH, Bi. Laura Musonye amesema ziara yao nchini Tanzania ni kuangalia jinsi huduma za afya zinavyotolewa ili kukabiliana na changamoto za mifumo ya utolewaji wa huduma za afya katika ngazi ya jamii.

Hata hivyo Bi. Laura ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuimarisha mifumo ya huduma za afya ikiwemo miundo mbinu, vifaa, vifaa tiba na huduma zinazotolewa katika vituo vya kutolea huduma za afya katika ngazi ya jamii.