Customer Feedback Centre

Ministry of Health

SERIKALI KUFANYA MABORESHO YA ADA YA LESENI ZA MADAKTARI

Posted on: February 15th, 2024



Na WAF - Dodoma.

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema Serikali itarejea upya na kufanya maboresho ya ada za leseni za madaktari chini ya Baraza la Madaktari Tanganyika (MCT)

Waziri Ummy ameyasema hayo Februari 14, 2024 wakati akifunga mkutano wa mwaka wa waganga wafawidhi wa vituo vya kutolea huduma za Afya ngazi ya msingi uliofanyika Jijini Dodoma ambapo Waganga hao walitoa ombi kwa Serikali kuona namna ya kupunguza gharama za leseni za udatkari wanazotakiwa kulipa.

“Ada mlikuwa mkilipa kila mwaka shilingi laki 100,000 na sasa hivi mnalipa shilingi laki 150,000 kwa miaka 2, tumshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alituelekeza tupunguze angalau imepunguza kwa kiasi na dhamira ya Serikali mmeiona kwa kupunguza ada za leseni lakini mimi na Naibu Waziri Mhe. Godwin Mollel tutaendelea kuwabana Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya na wa OR-TAMISEMI ili tuzidi kupunguza zaidi” amesema Waziri Ummy.

Waziri Ummy ameitaka MCT kutekeleza mipango ikatayowanufaisha zaidi wanachama wake ambao ni Madaktari kwa kuwa na mikakati endelevu ikiwemo kuwaendeleza kimasomo ikiwemo Ubingwa na Ubingwa bobezi pamoja na mafunzo ya muda mfupi.

Aidha amemuelekeza Naibu wa Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel kukaa na MCT kuangalia makusanyo na matumizi yao ili kuja na mpango kazi wa matumizi ya fedha hizo.