Customer Feedback Centre

Ministry of Health

SEKTA YA AFYA KUENDELEA KUWEKA KIPAUMBELE AJENDA YA KUPUNGUZA VIFO VYA MAMA NA MTOTO

Posted on: January 15th, 2024


Na. WAF - Dodoma


Sekta ya Afya kuendelea kuweka kipaumbele ajenda ya kupunguza vifo vya mama na mtoto katika vikao vinavyofanyika ngazi zote za Mkoa ili kuendelea kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi ikiwa ni malengo ya Taifa na Dunia. 


Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule leo Januari 15, 2024 Jijini Dodoma wakati akifungua kikao kazi chenye lengo la kujadili mikakati ya kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi, mama na watoto.


“Kupunguza vifo vya mama na mtoto ni malengo ya Dunia lakini pia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni dhamira yake hivyo sisi watendaji wake ni lazima tupambane nayo kwa kumuunga mkono Rais na Dunia kwa ujumla.” Amesema Mh. Senyamule.


Amesema, ni vyema Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Kijiji awe anashiriki vikao vya kikanuni katika ngazi zote za Halmashauri ili aweze kutoa taarifa ya hali ilivyo juu ya vifo vinavyotokea pamoja na changamoto zake.


“Kama kuna mama mjamzito ambae hafiki katika vituo vya kutolea huduma za Afya tupate taarifa ili watendaji wa Wilaya na Kijiji wazidi kutoa rai na kuelimisha kupitia mikutano yao ya hadhara kwa wananchi.” Amesema Mhe. Senyamule.


Aidha, Mhe. Senyamule ametoa wito kwa Waganga Wakuu wa Wilaya kupeleka taarifa za Wilaya juu ya vifo vya mama na mtoto kila wiki katika ofisi za Wakuu wa Wilaya ili kuwa na mkakati wa pamoja wa kuondoa vifo visivyo na ulazima kwa kushirikiana na wataalamu.


Katika hatua nyingine, Mhe. Senyamule amesema Serikali imedhamiria kupunguza tatizo la Kansa ya Uzazi kwa wanawake hivyo amewahimiza akinamama kujitokeza kupima ili waweze kupata matibabu haraka kwa kuwa huduma hiyo inatolewa bila malipo.


Kwa upande wake Mkurugenzi Idara ya Afya ya Uzazi Mama na Mtoto, Dkt. Ahmad Makuwani amesema Wizara ya Afya imeongeza kiwango cha watumiaji wa Vituo vya Afya wakati wa kujifungua na kufikia asilimia 81 ambapo 2016 tulikuwa na asilimia 63.


“Hii ina maana kwamba katika kila wajawazito 10, wajawazito 8 wanajifungulia katika Vituo vya kutolea huduma za Afya hivyo tumepunguza vifo vitokanavyo na uzazi kutoka vifo 556 katika kila vizazi hai Laki Moja hadi vifo 104 katika kila vizazi hali Laki Moja ambavyo vimepungua kwa asilimia 80". Amesema Dkt. Makuwani.