Customer Feedback Centre

Ministry of Health

RASILIMALI ZAIDI ZINAHITAJIKA KUPAMBANA NA UGONJWA WA MALARIA

Posted on: September 23rd, 2023

Na WAF, Newyork USA


Ili tuweze kuutokomeza ugonjwa wa malaria, tunahitaji rasilimali zaidi na uwajibikaji wenye kuleta matokeo chanya kwenye mapambano dhidi ya malaria.


Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu akiwa Jijini Newyork Marekani alipokuwa akiwasilisha taarifa ya mapambano dhidi ya Malaria kwa niaba ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Phillip Isdor Mpango kwenye kikao cha kujadili ufadhili wa mapambano dhidi ya malaria Afrika kupitia Umoja wa Viongozi wa Afrika katika Mapambano dhidi ya Malaria (ALMA)


“Tunahitaji rasilimali zaidi kupambana na Malaria, ugonjwa huu unaathiri asilimia 1.3 ya ukuaji wa uchumi Barani Afrika ni lazima sasa tuwekeze zaidi na kuwajibika kwenye mapambano dhidi ya malaria kwa kushirikiana na wadau wengine” Amesema Waziri Ummy.


Waziri Ummy amesema kuwa Tanzania inaendelea kujiimarisha kiuchumi kutokana na athari za janga la UVIKO-19 hivyo ni dhahiri kwamba rasilimali zinahitajika zaidi ili kuweza kufikia malengo ya kupambana na malaria.


Waziri Ummy amesema Tanzania inaendelea kuweka mkazo zaidi kwenye mapambano dhidi ya Malaria kwa kushirikiana na Sekta binafsi, Asasi za kiraia na Jamii kwa ujumla juu ya kukabiliana na ugonjwa wa Malaria.


“Tunashirikiana kwa ukaribu na Umoja wa Wabunge wanaopambana na Malaria pamoja na Magonjwa yasiyopewa Kipaumbele (TAPAMA) kuleta utashi wa kisiasa na ili wawe mabalozi wa kuelimisha na kuhamasisha zaidi jamii kwenye mapambano dhidi ya Malaria” Amesema Waziri Ummy.


Pamoja na hayo Waziri Ummy amebainisha kuwa Tanzania hivi karibuni imezindua Baraza la Kutokomeza Malaria ambalo lina jukumu la kuhamasisha upatikanaji wa rasilimali zaidi, kuelimisha jamii dhidi ya Ugonjwa huo ili kuongeza nguvu zaidi za mapambano dhidi ya Malaria.


“Tanzania, Afrika na Dunia nzima inaweza kuwa salama zaidi bila ya ugonjwa wa Malaria endapo kutakuwa na umoja kwenye mapambano dhidi ya ugonjwa huu” amesema Waziri Ummy Mwalimu.