Customer Feedback Centre

Ministry of Health

RAIS SAMIA ATOA MIL. 2 KWA MARIAM ANAYESAIDIA WATOTO NJITI KWA KUWAPA JOTO

Posted on: July 20th, 2023

Rais wa Jmahuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za pongezi na zawadi ya fedha taslimu kiasi cha Tsh Milioni 2 kwa Mariam Mwakabungu (25) anayejitolea kukumbatia watoto njiti katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Amana Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na wanahabari Julai 19, 2023 Mganga Mfawidhi wa Amana Dkt. Bryson Kiwelu amesema kuwa watu mbalimbali wameguswa na anachokifanya Bi. Mariam akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ameweka kipaumbele chake hasa uboreshaji wa Huduma za Afya Uzazi, Mama na Mtoto.

"Rais ametoa Shilingi Milioni 2 fedha taslimu kumpatia mama huyu kwa kujitoa kwake na amewapongeza viongozi wa Wizara ya Afya na Amana kwa ubunifu huu na uthubutu wa mama huyu kuwa sehemu yetu” amesema Dkt. Kiwelu.

Mara baada ya kupata habari hizo Bi. Mariam amesema kuwa anajisikia furaha na kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuguswa na huduma anayoitoa kwa watoto njiti katika Hospitali ya Amana.

“Sikutegemea nimeona kama ndoto Mimi nilikuwa najitolea tu nimeona kama jambo dogo kwangu niliona tu kama jambo la kawaida sikujua kama litafikia huku" amesema Mariam huku akibubujikwa na machozi ya furaha.

Mariam anasema kuwa hadi sasa amesadia watoto watatu kwa kuwakumbatia kwa siku nzima ili wapate joto linalowasaidi kuongeza uzito wao.

Kwa upande wake mdau wa Sekta ya Afya upande wa Huduma za Afya ya Uzazi na Watoto njiti, Mkurugenzi wa Taasisi ya Doris Mollel, Bi Doris Mollel amesema kuwa kitendo alichokifanya Mariam ni cha utu na ametoa mchango mkubwa katika kuokoa maisha ya watoto hao.

“Nampongeza sana Mariam, bado ni mdogo angeweza kufanya shughuli nyingine lakini ameguswa kusaidia watoto hao njiti, kitendo cha kukaa na mtoto kumpa joto hadi aweze kufikisha kilo 2.5 aje ahudumie mtoto mwingine kwa kweli ni kitendo cha kuthaminiwa, kuheshimiwa na kuigwa” amepongeza Dorris.

“Nawapongeza pia Hospitali ya Amana kwa kumruhusu Mariam kuja hapa na kuweza kutoa huduma hii ya kuwapa joto hawa watoto” amesema Dorris Mollel.