Customer Feedback Centre

Ministry of Health

RAIS DKT. SAMIA ACHAGIZA MAPAMBANO DHIDI YA MAAMBUKIZI MAPYA YA VVU.

Posted on: November 1st, 2023


Na WAF - Ulanga, Morogoro 


Tanzania chini ya Uongozi wa Dkt Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Afya, imekuwa kati ya nchi zinazoonyesha mafanikio katika kupambana ya maambukizi mapya ya VVU kwa kiwango kikubwa. 


Kauli hiyo imetolewa na mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Mahenge, ambaye ni Afisa Tawala wa wilaya Mahenge, Huruka Rajabu wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Jikubali katika viwanja vya Mapinduzi wilayani Mahenge katika Mji wa Ulanga, Novemba 1, 2023.


Amesema kuwa wilaya hiyo imeongeza maeneo ya kutolea huduma za ushauri nasaha na upimaji wa VVU na Huduma rafiki kwa Vijana ikiwa ni kuunga Mkono wa jitihada za Kupambana na Ugonjwa.


 "Serikali imeendelea kuimarisha mapambano kwa kutenga fedha za Ujenzi wa Vituo vya kutolea Huduma za Afya pia huduma ya upimaji inapatikana hata kwenye maeneo yenye viashiria vya maambukizi ya vvu kama vile kumbi za starehe, Nyumba za wageni, kwenye mabwawa na machimbo ya madini" amesema Huruka Rajabu


Ameongeza moja ya mambo ambayo pia serikali wilayani hapo inafanya na kuongeza idadi ya watu wanaotambua hali zao na upatikananji wa Huduma Rafiki


"Nitoe rai kwa vijana wote wajitokeze kwa wingi katika huduma za upimaji wa VVU kwa hiari ili wale watakaogundilika kuwa wana maambukizi ya VVU waweze kuanza dawa za ARV mapema ili watimize ndoto zao" ametoa wito Huruka 


 Kwa upande wake Mhandisi wa wilaya hiyo Amiri Mbuye akizungumza kwa niaba Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Mahenge, amesema kupitishwa kwa sheria ya upimaji VVU ambayo imepunguza umri wa vijana wanaotakiwa kupima VVU kwa ridhaa ya mzazi au mlezi kutoka miaka 18 hadi 15, na pia kuruhusu huduma za upimaji binafsi wa VVU, itasaidia kuwawezesha Vijana Kutambua hali zao za Maambukizi na Kuchukua Hatua stahiki za kujilinda.