NGUVU IONGEZEKE ILI KUKABILIANA NA MPOX TUNDUMA
Posted on: August 22nd, 2024
Na, WAF - Tunduma, Songwe
Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel ameutaka uongozi wa mkoa wa Songwe katika mpaka wa Tunduma kuongeza nguvu katika rasilimali watu na vifaa kwa ajili ya kuangalia mwenendo wa udhibiti wa magonjwa ya mlipuko ukiwemo Mpox.
Dkt. Mollel ameyasema hayo leo Agosti 22, 2024 wakati alipotembelea Forodha ya mpaka wa Tunduma Mkoani Songwe kwa ajili ya kuangalia hali ya utayari na kukabiliana na Ugonjwa wa Mpox
“Tunduma ni mpaka mkubwa hivyo tunatakiwa kuwapa nguvu zaidi ili kuwatengenezea nguvu ya wao kufanya vizuri zaidi katika kuangalia na kukabiliana na ugonjwa wa Mpox” Amesema Dkt. Mollel
Aidha Dkt. Mollel amesisitiza juu ya umakini wa watumishi katika kutoa taarifa sahihi ambazo hazitaleta taharuki kwani taarifa zote ambazo zitatolewa ziwe ni zenye uhakika bila ya kuficha endapo kutabainika kuna dalili.
“Mapokeo ya taarifa ambazo si rasmi zinaweza kuleta taharuki kubwa wakati si ugonjwa wenyewe, taarifa za kudhania sio nzuri ni lazima tuthibitishe kwa kupima kila kitu na endapo tutapata mtu tusifiche bali tuseme ukweli bila kudhani na baadae kupotosha kwa dhana tuliosema”. Amesema Dkt. Mollel
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Kinga Dkt. Vida Mbaga amesema watumishi wa Afya katika eneo la Mpakani Tunduma kuwa mabingwa wa kutoa taarifa zenye usahihi ili kuweza kukabiliana kwa haraka na namna ya kuweza kuudhibiti ugonjwa wa mlipuko