NENDENI MKAWE CHACHU YA MABADILIKO, MKATOE ELIMU KWA WENGINE
Posted on: April 21st, 2026Na Hassan Kimweri, WAF - Dar es Salaam
Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe, amewataka wahitimu wa mafunzo ya 'Field Epidemiology Frontline' kuwa chachu ya mabadiliko katika maeneo yao ya kazi na jamii kwa kutumia maarifa waliyoyapata katika kukabiliana na changamoto za afya.
Dkt. Magembe amesema hayo leo Aprili 17, 2026 wakati akizungumza kwenye hafla ya mahafali ya 22 ya wahitimu hao, yaliyofanyika katika Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS) jijini Dar es Salaam.
"Mafunzo hayo yamekuja wakati muafaka ambapo Afrika na Dunia inaendelea kushuhudia milipuko mbalimbali ya magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza," amesema Dkt. Magembe
Amesema, Serikali inaendelea kuimarisha uwezo wa wataalamu wa afya nchini ili waweze kufanya uchunguzi wa haraka, kuchambua taarifa sahihi na kutoa majibu stahiki pale changamoto zinapojitokeza katika jamii.
“Tunawahitaji wataalamu wenye uwezo wa kutumia takwimu, kutafsiri mwenendo wa magonjwa na kutoa tahadhari mapema kabla hali haijawa kubwa zaidi,” amesema Dkt. Magembe.
Aidha, Dkt. Magembe amesisitiza umuhimu wa kutumia takwimu na taarifa zinazokusanywa katika vituo vya afya, hospitali na ngazi mbalimbali za jamii, akieleza kuwa taarifa hizo zina mchango mkubwa kwa Serikali katika kupanga mikakati ya kudhibiti magonjwa.
ameeleza kuwa, Mbali na kuwa na wataalamu wenye elimu ya juu, Dkt. Magembe amesema, bado kuna umuhimu mkubwa wa kuwawezesha watumishi wa mstari wa mbele ambao ndiyo hukutana moja kwa moja na wananchi katika utoaji wa huduma za afya.
Akihitimisha hotuba yake, Dkt. Magembe amewapongeza wahitimu hao kwa juhudi zao na kuwahimiza kuendelea kujifunza na kutumia maarifa yao kwa manufaa ya taifa na kuwafundisha wengine, kushirikiana na jamii pamoja na kusaidia kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji wa magonjwa.