Customer Feedback Centre

Ministry of Health

MUHIMBILI NYINGINE KUJENGWA KIGOMA.

Posted on: July 6th, 2023

Na WAF Kigoma.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango amesema Serikali imedhamiria kujenga hospitali ya Rufaa ya kanda ya Magharibi yenye hadhi sawa na hospitali ya Taifa Muhimbili itayosaidia kuondoa changamoto ya Rufaa za wagonjwa waliokuwa wakitibiwa katika hospitali za Rufaa za Mbeya, Benjamin Mkapa na Muhimbili.

Dkt. Mpango amesema hayo wakati akizindua hotel ya Bwami Dubai iliyopo Kasulu Mkoani Kigoma, ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kuzindua miradi mbalimbali Mkoani Kigoma.

"Pale Kigoma tunajenga hospitali ya kanda, lakini sio hivyo tu vyuo vikuu mnasikiaga vipo Dar es Salaam, kwahiyo chuo kikuu cha tiba Muhimbili wamekuja kuanzisha tawi la chuo kikuu Kigoma na kitakuwa sambamba na hiyo hospitali ya kanda." Amesema.

Ameendelea kusema, pamoja na kujengwa kwa Zahanati ya Kasumo bado Serikali iliona haja ya kuwa na hospitali hiyo ya kanda ili wananchi wa Mkoa wa Kigoma pamoja na nchi za jirani waweze kunufaika na huduma hizo jambo litalosaidia kupunguza Rufaa katika Mikoa ya Dodoma.

Aidha, Mhe. Dkt. Mpango ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa huo kuwalisha watoto lishe inayofaa kwa afya ili kuwaongezea uwezo wa akili, huku akiwataka Wataalamu wa masuala ya lishe kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kuwapa lishe bora watoto ili kuinua kiwango cha elimu kwa watoto wao.

Naye Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amesema, katika Sekta ya Afya kuanzia ngazi ya Hospitali ya Mkoa mpaka zahanati Mkoa umepokea kiasi cha Shilingi Bilioni 49 iliyosaidia kununua vifaa tiba vya kisasa, kuboresha miundombinu ya kutolea huduma ili wananchi wa Kigoma wapate huduma bora.

Amesema, kwa uwekezaji mkubwa wa Trilioni 1.3 uliopewa na Serikali ya Rais Samia katika Sekta ya Afya umesaidia kupunguza Rufaa za wagonjwa kwenda kutibiwa nje ya nchi, na kusisitiza uwekezaji huo umesaidia kuongeza idadi ya wagonjwa kutoka nje ya nchi wanaokuja kutibiwa ndani ya Tanzania (medical tourism).

Mwisho.