Customer Feedback Centre

Ministry of Health

MNH- MLOGANZILA YAFANYA UPASUAJI WA KIBINGWA BOBEZI KUPUNGUZA UZITO ULIOPITILIZA

Posted on: November 1st, 2023


Na WAF

Hospitali ya Taifa Muhimbili -Mloganzila imefanya upasuaji wa kibingwa bobezi wa kupunguza uzito kwa watu wanne wenye uzito uliopitiliza ikiwa ni kwa mara ya kwanza nchini na kuandika historia katika Hospitali za umma nchini.


Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Mohamed Janabi wakati akiongea na wanahabari huku akisema upasuaji huo umefanyika kwa utaalamu wa hali ya juu ambapo waliopata huduma hiyo hakuna aliyepasuliwa bali wametumia kifaa maalum (endoskopia) kuingia katika tumbo na kupunguza sehemu ya tumbo la chini na pia kutumia matundu madogo.


Prof. Janabi ameongeza kuwa huduma hii imehusisha wataalamu wa hospitali kwa kushirikiana na Daktari Bingwa wa Upasuaji kutoka nchini India, Dkt. Mohit Bhandar pamoja na Taasisi ya MedINCREDI, ambapo baada ya kufanyiwa upasuaji huo atapunguza uzito takribani kilo 20 hadi 30 kwa kipindi cha mwaka mmoja.


“Tuliowafanyia huduma hii wana umri wa kati ya miaka 36-40, ambao uzito wao ni kati kilo 107 hadi 142, mmoja aliruhusiwa baada ya masaa nane na wengine watatu waliruhusiwa siku iliyofuata hivyo ukifanyiwa huduma hii haikuzuii kurudi katika majukumu yako kwa wakati”. Amebainisha Prof. Janabi.


Aidha, Prof. Janabi ameishauri jamii kujikinga kupata uzito uliopitiliza kwa kuepuka kula mara kwa mara kwakuwa uzito unaweza kusababisha magonjwa yasiyoambukiza ambayo gharama zake za matibabu ni ghali kuzimudu ikiwa hujajiunga na mfuko wa bima ya afya.


Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Upasuaji MNH-Mloganzila, Dkt. Eric Muhumba amesema huduma ya kupunguza uzito ina faida mbalimbali ikiwemo kuepuka magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo kisukari, shinikizo la juu la damu, saratani, magonjwa ya moyo na kiharusi ambayo ni tishio duniani.