Customer Feedback Centre

Ministry of Health

MGANGA WA JADI AJISALIMISHA KWA MADAKTARI BINGWA WA RAIS SAMIA

Posted on: June 19th, 2024


Ameishi na Uvimbe kwa zaidi ya miaka 20


Na WAF, KWIMBA


BI Shamizi Mwanamalunde Mganga wa tiba asili, mkaazi , wilayani Kwimba mkoani Mwanza amefanyiwa upasuaji na kutolewa uvimbe wenye uzito wa Kilo 2.5 aliodumu nao kwa zaidi ya miaka 20.


Akiongea Hospitalini hapo Juni, 19, 2024 mara yakupatiwa matibabu amesema uvimbe huo ulianza kama mimba ya miezi miwili lakini haikuendelea kukua tangu kipindi hicho.


“Sikumbuki ni mwaka gani lakini mwanangu wa kike alikuwa darasa la tano na hivi sasa alisha maliza shule na kuolewa na ana watoto wanane kwa sasa”. amesema Bibi MwanaMalunde.


Bibi MwanaMalunde ameongeza kuwa pamoja na kwamba yeye mwenyewe ni Mganga wa tiba asili lakini hakuweza kujiganga katika kipindi chote hicho.


“Niliposikia wamekuja hawa wataalam wa Samia, nilifurahi nikaja wakanipima vizuri na wakanipasua kutoa liuvimbe” ameongeza Bi Malunde


Kwa upande wake Mganga mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya Dkt. Neema Gervas amesema kambi ya Madaktari Bingwa wa Samia imekuwa na matokeo chanya.


“Siku za kawaida huwa tunapokea wagonjwa 60 hadi 70 lakini ujio wa Madaktari Bingwa umeongeza mahudhurio hadi kufikia 120 hadi 130” Amesema Dkt. Neema na kuongeza tunatumia fursa hii pia kuwajengea uwezo watu wetu.


Naye Daktari Bingwa wa Upasuaji Lesso Mwinyimkuu amesema toka kuanza kambi hiyo wamefanikiwa kufanya upasuaji kwa wagonjwa Wanane


“Tumekuwa na upasuaji ndogo mbili na upasuaji mkubwa ambao ungehitaji rufani ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa au Kanda zilikuwa sita” amesema Dkt Mwinyi Mkuu


Madaktari Bingwa wa Mama Samia wapo mkoani Mwanza kwa siku tano kuanzia Juni 17 hadi 21, 2024 kwa ajilj ya huduma za kibingwa na Bobezi kwa Halmashauri zote nane za mkoa huo.


MWISHO