MCHENGERWA ATOA WITO KUIMARISHA USHIRIKIANO KUPUNGUZA AJALI ZA BARABARANI
Posted on: April 20th, 2026Na. Aisha Swahibu, WAF - Dar es Salaam
Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa ametoa wito kwa Taasisi na wadau wa maendeleo ya sekta ya afya kushirikiana kwa karibu ili kukabiliana na ongezeko la ajali za barabarani, tatizo linaloendelea kugharimu maisha ya maelfu ya watu kila mwaka.
Waziri Mchengerwa, ameyasema hayo leo Aprili 16, 2026 wakati akimkaribisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Pili wa Shirikisho la Jumuiya ya Madaktari bingwa wa upasuaji wa Ubongo, Mgongo na Mishipa ya Fahamu, jijini Dar es salaam
Amesem kuwa, ongezeko kubwa la usajili wa vyombo vya moto, hususan pikipiki, limechangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa ajali na vifo .
“Takwimu zinaonesha kuwa kiwango cha vifo barani Afrika kimefikia wastani wa watu 26.6 kwa kila 100,000, kiwango kinachozidi wastani wa dunia wa watu 15 kwa kila 100,000,” amesema Mhe. Mchengerwa
Mhe. Mchengerwa amebainisha kuwa hali hiyo inaashiria dharura ya kuchukua hatua madhubuti, hasa ikizingatiwa kuwa, takribani asilimia 97 ya ajali hizo husababishwa na makosa ya kibinadamu.
“Suluhisho la kudumu linahitaji ushirikiano wa sekta mbalimbali, ikiwemo elimu kwa vijana ambao wako hatarini zaidi, kuimarisha sheria za usalama barabarani, pamoja na kuboresha miundombinu ya barabara,” amesema Mhe. Mchengerwa
Mhe Mchengerwa amesisitiza“Ni lazima tushirikiane kama taifa na kama bara la Afrika ili kupunguza ajali hizi. Elimu sahihi kwa vijana, utekelezaji madhubuti wa sheria, na uwekezaji katika miundombinu ni mambo ya msingi katika kukabiliana na changamoto hii,”