Customer Feedback Centre

Ministry of Health

MATUMIZI YA VYOO BORA YAMEONGEZEKA NCHINI TANZANIA

Posted on: November 19th, 2023



Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema Tanzania imekua na ongezeko kubwa la watu wanao tumia vyoo bora kutoka asilimia 21 mwaka 2016 hadi asilimia 74.8 mwaka 2022 ambapo ni hatua chanya ya kufikia lengo la 6.2 la Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Dunia ya 2030 “Sustainable Development Goals”.


Waziri Ummy amesema hayo katika tamko lake likionesha hali ya matumizi ya vyoo nchini ambapo mikoa inayoongoza kwa matumizi ya vyoo bora ni Dar es Salaam (98.5%), Ruvuma (92.1%) na Njombe(87.6%).


Aidha, Waziri ummy amesema Licha ya kuwa tumepiga hatua kwenye kiashiria hicho bado kuna baadhi ya watu hawatumii vyoo ambapo takwimu zinaonesha kuwa asilimia 9.8 ya watu nchini hawana vyoo kabisa ambapo hali ni mbaya zaidi maeneo ya vijijini.


“Kwa mujibu wa taarifa hii asilimia 13.4 ya wakazi wa vijijini hawana vyoo kabisa. Tafsiri ya kiashiria hiki ni kwamba watu hawa ndiyo wanaojisaidia ovyo (Open defecation) vichakani na maeneo mengine ambayo sio rasmi. Hali hii inachangia kuwepo kwa magonjwa ya milipuko ikiwemo kipindupindu ambapo kwa kipindi cha Januari hadi Oktoba 2023 jumla ya watu 749 waliougua na 16 kupoteza Maisha”. Amesema Waziri Ummy.


Hata hivyo Waziri Ummy amebainisha mikoa inayoongoza kwa kutokuwa na vyoo ni Katavi (24.3%), Simiyu (24.3%) na Manyara (22.3%) huku akiagiza Sekretatarieti za Mikoa na Halmashauri kuhakikisha kaya zote nchini zinakuwa na vyoo bora.


Waziri Ummy ameielekeza Mikoa na Halmashauri kutekeleza kufanya ukaguzi kwenye kaya, sehemu za Jumuiya, maeneo ya biashara na Taasisi zote kwa kuhakikisha zinajenga na kutumia vyoo bora pia Kusimamia vyema Sheria ya Afya ya Jamii na Sheria Ndogo zinahusiana na ujenzi na matumizi ya choo bora kwenye ngazi ya Kaya, Taasisi na maeneo ya Jumuiya.


Vile vile ameelekeza kuhakikisha zinasimamia vyema matumizi ya vyoo kwa wasafiri wawapo safarini kwa kuhakikisha mabasi yanasimama kwenye maeneo rasmi ikiwemo stendi za mabasi na vituo maalum pamoja na kupiga marufuku tabia ya wasafiri kujisaidia hovyo maarufu kama kuchimba dawa kwani ni aibu kwa Taifa na pia udhalilishaji wa utu.