Customer Feedback Centre

Ministry of Health

MASHINE YA KISASA YANUSURU MENO 14 HOSPITALI YA WILAYA NYASA KUNG'OLEWA

Posted on: November 3rd, 2024

Na WAF - NYASA

Timu ya Madaktari Bingwa wa Rais Samia wilayani Nyasa mkoani Ruvuma na imefanikiwa kuzindua huduma mpya ya kinywa na meno katika Hospitali ya wilaya na kuokoa meno ya watu 14 ambayo yangeng’olewa kama kusingekuwa na mashine husika.

Hayo yamesemwa Novemba 2, 2024 na Daktari bingwa wa kinywa na meno Luciana Albert kutoka hospitali ya Taifa Muhimbili alipokuwa akitoa mrejesho wa huduma walizozitoa kwenye kambi ya siku sita wilayani Nyasa.

"Kwa watu wanaohitaji huduma ya meno ni wengi, lakini kwa kipindi kifupi hiki nimeonana wagonjwa ambao pengine kusingekuwa na mashine hii ya kisasa wangelazimika kung’olewa meno yao kitu ambacho hatushauri sana,” amesema Dkt. Albert.

Dkt. Albert amesema huduma hiyo ya kinywa na meno iliyoanzishwa itaendelea kufanya kazi na wananchi waendelee kuhudhuria hospitali kwa ajili ya uchunguzi wa meno na waondoe hofu kwani huduma zimeimarika na vifaa tiba vipo vya kisasa.

“Tokea tumeanze kwa mara ya kwanza huduma hii hapa Hospitalini watu wamejitokeza ingawa siku ya kwanza mwitikio haukuwa mkubwa lakini hadi tunafunga kambi wagonjwa walikuwa ni wengi na tumewahudumia vizuri,” amesema Dkt. Albert.

Kambi hiyo ya siku sita ilianza jumatatu ya tarehe 28, Oktoba na kuhitimishwa leo tarehe 02 Novemba, pamoja na kutibu wagonjwa wahudumu wa sekta ya Afya wamejengewa uwezo wa kibingwa katika hospitali hiyo.