Customer Feedback Centre

Ministry of Health

MAKAMU WA RAIS WA TANZANIA AZINDUA HUDUMA YA M-MAMA MOUNT MERU.

Posted on: June 22nd, 2023

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango Juni 22, 2023 azindua huduma ya mfumo wa rufaa na usafirishaji wa dharura kwa mama mjamzito, aliejifungua na mtoto mchanga katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha ikiwa ni kati ya Mikoa 16 inayotoa huduma hiyo nchini Tanzania.

Akizungumza katika hafla hiyo, ameeleza kuwa Tanzania inatekeleza mkakati wa kuboresha Afya ya uzazi, mama na mtoto na lishe ambapo una lengo la kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi hadi kufikia mia moja kati ya vizazi hai laki moja na vifo vya watoto wachanga vibakie kumi na sita kati ya vizazi hai elfu moja itakapofika mwaka 2025. Ametaja kuwa mojawapo ya changamoto zinazosababisha vifo vya watoto wachanga ni kuchelewa kufika kwenye vituo vya kutolea huduma na kupata huduma stahiki hasa maeneo ya vijijini.

Mfumo huu wa M- mama tangu umeanzishwa hapa Mkoani Arusha Aprili 2023 mpaka Juni 20, 2023 tayari umeshasafirisha jumla ya dharura 607 kati ya hizo asilimia 82 zilikuwa dharura za wakina mama na asilimia 18 zilikuwa dharura za watoto wachanga aidha asilimia 93.7 za wagonjwa wote waliosafirishwa yalitumika magari ya wagonjwa ya serikali na hakukuwa na rufaa kwenye ngazi ya jamii.

Vilevile Serikali inaendelea kuajiri wahudumu wa Afya na hivi sasa imepeleka wataalamu 100 katika vituo zaidi 40 ili kuwajengea uwezo watoa huduma za Afya kutoa huduma zenye ubora unaostahili na mpango huu utakuwa endelevu ili kuhakikisha inawafikia watoa huduma wengi zaidi na kuhakikisha wakina mama na watoto wanapata huduma bora wanapofika hospitali.

Mfumo huu wa dharura wa M-mama ulioagizwa utekelezwaji wake na Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan unafanya kazi katika Mikoa 16 ya Tanzania bara Shinyanga, Mtwara, Lindi, Morogoro, Arusha, Manyara, Singida, Dodoma, Simiyu, Kilimanjaro, Tanga, Mwanza, Mara, Mbeya, Songwe na Rukwa na Mikoa yote mitano ya Zanzibar.

MWISHO