MAFUNZO YA DHARURA YAONGEZA UFANISI HOSPITALI YA BUHIGWE
Posted on: April 23rd, 2026Na. Happyness Hans WAF - Kigoma
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Buhigwe, Dkt. Baraka Kemelo amesema hospitali imepokea wataalamu kutoka Wizara ya Afya kwa lengo la usimamizi shirikishi na kutoa mafunzo ya huduma kwa wagonjwa wa dharura na mahututi pamoja na kukagua matumizi ya jengo la dharura ili kuhakikisha linatumika ipasavyo.
Ameeleza hayo leo Aprili 23, 2026 katika Hospitali ya Wilaya ya Buhigwe, amesema kuwa mafunzo hayo yamewanufaisha watumishi, hasa kwa kuwajengea uwezo wa kutoa huduma za dharura na kuimarisha watumishi wapya, sambamba na kupewa mwongozo wa upangaji sahihi wa vifaa na matumizi ya vyumba.
Aidha, ameomba mafunzo hayo yawe endelevu ili kuongeza ufanisi zaidi hususan kwa watumishi wapya kuweza kukabiliana na changamoto za huduma za dharura.
Kwa upande wake Muuguzi wa Hospitali hiyo, Elizabeth Mlai, amesema mafunzo waliyopata yameboresha utendaji wao katika kitengo cha dharura na ajali, amebainisha kuwa wamejifunza matumizi sahihi ya mashine za kupumulia (ventilator), muhimu kwa wagonjwa mahututi.
Ameongeza kuwa awali walikuwa na uelewa mdogo, lakini sasa wana ujuzi wa kutosha, Hali itakayosaidia kuboresha huduma, kuokoa maisha na kupunguza rufaa zisizo za lazima.
Naye, Afisa tabibu wa hospitali hiyo Makanja Malima, akihitimisha amesema wataalamu kutoka Wizara ya Afya wamewajengea uwezo wa kutumia vifaa tiba na mashine za kisasa. Pia wameelekezwa namna bora ya kupanga dawa na vifaa katika jengo la dharura hivyoa ameishukuru Wizara kwa kuratibu zoezi hilo na kuomba mafunzo hayo yaendelee ili kuwasaidia kuongeza ujuzi na kuboresha huduma kwa wananchi.