Customer Feedback Centre

Ministry of Health

MADAKTARI WA MAMA" WASAIDIA KUOKOA MAISHA YA MAMA NA MTOTO KITANGARI

Posted on: June 19th, 2023



"Nilifika hapa Kituo cha Afya Kitangari Wilaya ya Newala Mkoa wa Mtwara nikiwa katika hatua za mwisho za ujauzito, ilibainika kuwa nina tatizo la shinikizo la juu damu hivyo ilitakiwa nisaidiwe haraka kwa kuwa maisha yangu na ya mtoto yalikuwa hatarini, hofu ilinijaa moyoni kutokana na hadhi ya kituo hiki".

Hivyo ndio anavyoanza kusimulia Bi. Veronica Marco Benjamini akiwa na sura ya bashasha huku amempakata mtoto wake wa kiume mwenye umri wa siku moja.

Bi. Veronica anaeleza kuwa huo ni uzao wake wa tatu ambapo watoto wawili waliotangulia aliwapata Mkoani Ruvuma katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo.

"Nilipata wasiwasi kuwa hiki ni kituo cha Afya tu, wataweza kweli kunisaidia? lakini niliona sura za wataalamu wapya ambao walinieleza kuwa wao wameletwa na Rais Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuja kitangari kuwasaidia wananchi lakini pia kuwafundisha wataalamu wa kituo hicho". Amesema Veronica

Ameongeza kuwa alifanyiwa upasuaji Juni 5 mwaka huu baada ya kushindwa kujifungua kawaida ambapo alitoka salama yeye na mtoto lakini bado wamesalia katika kituo hicho kwa uangalizi zaidi.

"Asante Mama kwa kutuletea madaktari Bingwa katika maeneo yetu, hakika umeleta mageuzi makubwa, naomba mpango huu uendelee Tanzania nzima ili kuokoa wamama na watoto". Ameeleza Bi.Veronica.

Kampeni ya "Madaktari wa Mama" inalenga kutekeleza azma ya Rais Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutokomeza vifo vya mama na mtoto, inaratibiwa na Wizara ya Afya ambapo imeambatanisha madaktari bingwa wa magonjwa ya Wanawake na Uzazi, Usingizi na Ganzi, Madaktari wa Watoto Wachanga na wauguzi wabobezi wamesambazwa katika mikoa 12 nchini ambapo wanawajengea uwezo wataalamu wa afya katika ngazi ya msingi Ili waweze kuwahudumia Wanawake na Watoto wanaozaliwa katika maeneo yao Ili kuweza kupunguza hatari ya vifo.

Mwisho