Customer Feedback Centre

Ministry of Health

MADAKTARI BINGWA WA MACHO WAWEKA KAMBI MBARALI KUFANYA UPASUAJI MTOTO WA JICHO

Posted on: August 15th, 2023

Na. Majid Abdulkarim, Mbarali

Madaktari Bingwa wa macho wameweka kambi ya wiki moja Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya kwa ajili ya kuwatafuta wagonjwa wenye matatizo ya mtoto wa jicho ambapo mpaka sasa wagonjwa 20 wamefanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho kwa siku ya leo.

Hayo yameelezwa na Meneja Mpango wa Taifa wa Huduma za macho kutoka Wizara ya Afya Dkt. Bernadetha Shilio wakati wa kliniki ya kuwatafuta wagonjwa hao wilayani humo ambapo amesema kambi hiyo imefadhiliwa na Shirika la Kimataifa la Helen Keller.

Dkt. Bernadetha amesema kambi hiyo ilianza Agosti 14 mwaka huu na inatarajiwa kuendelea wiki nzima huku wakiifanya nyumba kwa nyumba ili kubaini wagonjwa wenye tatizo la matoto wa jicho na kuwafanyia upasuaji.

Amesema mpaka sasa wamewafikia wagonjwa 800 ambapo amesema wanatarajia kufanya upasuaji kwa macho 500 kwani kuna baadhi wanaweza kufanyiwa macho yote mawili.

Meneja huyo amesema mpaka sasa wamefanya upasuaji kwa wagonjwa 20 na wengine wanaendelea na uchunguzi ili huduma ya upasuaji iweze kuendelea kutokana na uchunguzi wa awali utakao kuwa umefanyika.

“Huduma hii ni ya kipekee kidogo kwa sababu wagonjwa hawa wanatafutwa kwenye nyumba zao wakipatikana wanafanyiwa uchunguzi wa awali halafu wanakuja kwenye kambi kabla ya kufanyiwa upasuaji,”amesema Dkt. Bernadetha.

Amesema madaktari wawili bingwa kutoka Hospitali ya Kanda ya Mbeya pamoja na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya kwa pamoja wanashirikiana katika kufanya upasuaji na tayari walipata mafunzo ya ziada kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa wengi katika kipindi kifupi lakini kwa matokeo mazuri zaidi.

Amesema wanashukuru tangu upasuaji huo umeanza zaidi ya asilimia 80 ya wagonjwa wanapata matokeo mazuri na wagonjwa wametoa ushuhuda wa hilo.

Vile vile ameeleza kuwa wanalenga kufika katika mkoa wa Njombe kwa ajili ya kuwafanyia upasuaji wagonjwa watakao bainika kuwa na tatizo la mtoto wa jicho.

Ameweka wazi kuwa wanaopata ugonjwa wa mtoto wa jicho ni wazee na wanakosa watu wa kuwasindikiza kwa kuzingatia kwamba hawaoni kwahiyo huduma hiyo inawakomboa na kuwasaidia kushirikiana na jamii