MADAKTARI BINGWA 37 WA RAIS SAMIA WATUA MKOA WA IRINGA.
Posted on: October 28th, 2024Na WAF, Iringa
Timu ya Madaktari Bingwa 37 wa Rais Samia inayozunguka nchi nzima kwa ajili ya kutoa huduma za Kibingwa imewasili katika Mkoa wa Iringa na kuweka kambi ya muda wa wiki moja kuanzia Oktoba 28 hadi Novemba 1, 2024 katika Halmashauri zote za Mkoa wa Iringa.
Akiwakaribisha Mkoani hapo Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa huo Bw. Venance Ntiyalundura amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuona umuhimu wa kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi.
“Kwa namna ya pekee namshukuru sana Rais wetu Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuona umuhimu wa kusogeza huduma karibu na wananchi, ni ukweli ulio wazi wananchi wanapata changamoto wakati wanapohitaji huduma bobezi kwani huwalazimu kisafari kwenda Muhimbili au KCM na wakati mwingine baadhi yao hushindwa kufika hata hospitali ya rufaa hapa Iringa kupata huduma, sasa huduma zinawafuata huko walipo,“ amasema Kaimu Katibu Tawala
Aidha amewataka wananchi wa mkoa huo wenye changamoto za kiafya wafike kwa wingi kupata huduma hizo ambazo zinapatikana katika hospitali za wilaya zilizpo katika mkoa huo .
“Natamani wananchi wafike kwa wingi mahali ambapo huduma zinatolewa kwani mama Samia anawajali wananchi wake ndiyo maana amesogeza huduma karibu na ameona changamoto wanazokutana nazo, hivyo ameamua madaktari ndiyo wawafuate wananchi walipo,”amesema Bw. Ntiyalundura.
Naye Mratibu wa programu hiyo kutoka Wizara ya Afya, Bi. Paskalina Andrea amesema lengo la ujio huo wa Madaktari Bingwa ni kusogeza huduma za kibingwa na Bobezi kwa wananchi.
Bi. Andrea amesema kuwa hiyo ni awamu ya pili ambapo awamu ya kwanza walizifikia hospitali za wilaya 184 katika mikoa 26.
“Tulipata mafanikio makubwa kwa kuwafikia wananchi zaidi ya elfu 70 na waliridhishwa na huduma, awamu ya pili tunategemea kuwafikia wananchi elfu kumi kwa kila halmashauri katika mkoa wa Iringa.
Aidha mratibu huyo ametoa rai kwa Madaktari hao kwenda kutoa huduma bora kwa wananchi ili kupunguza rufaa ya kwenda katika hospitali kubwa.