Customer Feedback Centre

Ministry of Health

KONGAMANO LA KISAYANSI LA TIBA ASILI KUTUMIKA KUBORESHA TIBA, TAFITI NA ELIMU YA TIBA ASILI NCHINI

Posted on: August 30th, 2023

Na WAF Dar Es Salaam


Kongamano la pili la Kisayansi la Tiba asili/Tiba Mbadala lenye washiriki zaidi ya 200 kutoka nchi nzima  litatumika kubadilishana taarifa, kubadilishana tafiti na kufungua maeneo mapya ambayo yatazidi kuonesha mchango wa Tiba asili nchini katika kuboresha Tiba na elimu ya Tiba Asili,


Yamesemwa hayo leo  na Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Prof. Pascal Rugajo akifungua Kongamano hilo katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar Es salaam ikiwa ni kuelekea kilele cha maadhimiaho ya Wiki ya Tiba Asili ya Muafrika yatakayofanyika Tarehe 31 Agosti katika viwanja vya Mnazi Mmoja


Prof Rugajo amesema kutokana na kongamano hili kutakuwa na maazimio mbalimbali ambayo  yatajadiliwa kuangalia namna gani yanaweza kuboresha zaidi Elimu ya Tiba Asili na huduma za Tiba mbadala nchini 


"Kongamano hili ni kusanyiko mahsusi ambalo limeleta wadau wote wa Tiba Asili wakiwemo Wanasayansi mbalimbali, vyuo na wawakilishi wa Waganga wa Tiba asili  na Tiba mbadala nchini ambalo litatumika kubadilishana taarifa na tafiti ili kufanya Serikali yetu kuona mchango wa Tiba asili nchini" amesema Prof. Rugajo 


Aidha Prof. Rugajo amesema mwaka huu tumeshuhudia Tiba asili ikipata nafasi katika Hospitali mbalimbali nchini, kuna Hospitali saba ambazo baada ya mafunzo kwa Madaktari na wafamasia  wameweza kupokea dawa zaidi ya 19 ambazo zinaendelea kutibu wagonjwa mbalimbali


"Mgonjwa atafika kwa Daktari ataonwa kwa njia za kisasa akifika mwisho ataambiwa kuna Dawa za Asili/Mbadala na Dawa za kizungu ambapo mgonjwa atachagua atumie ipi maana tiba asili ina mchango mkubwa na inapaswa kuendelezwa katika Utafiti, Mafunzo na Tiba yenyewe kwa ujumla" amesema Prof. Rugajo


Kwa upande wake mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binaadamu - NIMR, Prof Said Abood amesema jukumu kubwa la Taasisi hiyo ni kufanya tafiti za tiba asili na tiba mbadala kwa kuangalia ufanisi na masuala ya usalama na ubora wa Tiba Asili


"wito wangu kwa Waganga na watoa huduma za tiba asili Nchinj waje NIMR tushirikiane kufanya tafiti kama mtu yuko na Dawa ili kuhakikisha kama ipo salama na ina ufanisi unaotakiwa na waondokane na dhana kwamba wakileta dawa zao kwa ajili ya kufanyiwa utafiti kwamba zitaibiwa".