Customer Feedback Centre

Ministry of Health

KIPAUMBELE CHA KWANZA CHA RAIS SAMIA NI KUPAMBANA NA MAGONJWA HATARISHI KWA KUWALINDA WATUMISHI WA AFYA

Posted on: September 6th, 2023


Waziri Ummy amesema kipaumbele cha kwanza cha Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kupambana na magonjwa hatarishi na magonjwa ya mlipuko kwa kuwalinda watumishi wa afya.

 

Waziri Ummy amesema hayo akiongozea majibu ya swali la nyongeza lililoulizwa na Mheshimiwa Jackline Ngonyani Msongozi (Mbunge Viti Maalum Mkoa wa Ruvuma) leo bungeni kuhusu kuwalinda watumishi wa afya katika kutoa huduma kwa wagonjwa wa magonjwa ya mlipuko.

 

“Rais Samia Suluhu Hassan anatuwezesha kwa kutoa vifaa kinga vya kutosha kwa ajili ya watumishi wa afya, pale kunakotokea changamoto yoyote kwa mtumishi wa afya wakati wa kutoa Huduma serikali inafanya kila linalowezekana kuokoa maisha ya mtumishiwa huyo". Amesema Waziri Ummy.

 

Ameeleza kuwa kabla ya mtumishi wa afya kuanza kuhudumia mgonjwa wa magonjwa hatarishi na ya mlipuko anapewa mafunzo ya jinsi gani ya kuhudumia wagonjwa wa magonjwa hayo.

 

Akitoa mfano wakati wa mlipuko wa ugonjwa wa Marburg Mkoani Kagera amesema kuna mtumishi alipata changamoto ya kupata maambukizi lakini serikali ilifanya jitihada za kupeleka madaktari Bingwa saba na wauguzi bingwa pamoja na kupeleka mashine ya kusafisha figo kwa lengo la kuokoa maisha.

 

Aidha, Waziri Ummy amewashukuru watumishi wa afya na kuwatia moyo kwa kuendelea kutoa Huduma za afya kwa watanzania.